Katika hatua inayoonyesha wazi kuwa Serikali imesikia na
kujibu mahitaji ya haraka ya vijana (maarufu kama 'Gen Z') kuhusu elimu, ujuzi,
na ajira, Wizara Kuu kadhaa zimekutana Dodoma kuweka mikakati thabiti.
Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kuimarisha ushirikiano
ili kuwawezesha vijana wa Tanzania kupata fursa zinazokidhi mahitaji ya soko la
ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kikao hicho kilijumuisha ushirikiano mkubwa kutoka:Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana.
Kikao hicho kiliwekewa msukumo na viongozi waandamizi,
wakiongozwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa
Carolyne Nombo, na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Jenifa
Omolo.
Profesa Nombo alisisitiza jinsi Serikali inavyotumia mifumo
yake rasmi kujibu changamoto za vijana kuhusu ujuzi: Sera ya Elimu na Mafunzo
ya 2014, Toleo la 2023, pamoja na mitaala iliyoboreshwa, vinaendelea kumwandaa
kijana wa Kitanzania kupata ujuzi unaohitajika katika ulimwengu wa kazi.
Sera hiyo inatoa nafasi hata kwa vijana walioacha shule
awali kurejea na kupata elimu kupitia mfumo rasmi na usio rasmi.
Aidha Serikali inaendelea kupanua fursa za ufundi na
mafunzo ya ufundi stadi, kutoa mikopo ya elimu, pamoja na ufadhili kupitia
Samia Scholarship ili kuongeza wigo wa vijana kupata elimu na ujuzi.
Katibu Mkuu, Jenifa Omolo, aliipongeza Wizara ya Elimu kwa
kuanzisha programu hizi zinazolenga kuwawezesha vijana kujitegemea na
kushindana katika soko la ajira, akisisitiza kuwa programu hizo ni muhimu
kuchochea ushiriki wa vijana katika uchumi wa taifa.
Maazimio Makuu ya Ushirikiano
Ili kuhakikisha vijana wanapata taarifa sahihi na
kuunganishwa moja kwa moja na soko la ajira, viongozi hao wamekubaliana
kuimarisha maeneo yafuatayo:Upatikanaji wa taarifa,rasilimali fedha na
ushirikiano wa viwanda.
Kuimarisha upatikanaji wa taarifa za fursa kwa
vijana,Kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia mafunzo mahususi na
stadi za kisasa na Kuratibu programu zitakazowaunganisha vijana na viwanda ili
kupata mafunzo kwa vitendo (practical training) kumeelezwa ndio hitaji la
haraka la vijana kwa sasa.
Kikao hiki kinatoa ishara wazi kwamba Serikali inatambua
mchango mkubwa wa vijana na imedhamiria kuondoa vikwazo vinavyokwamisha
upatikanaji wao wa elimu bora na ajira.

0 Maoni