Wito umetolewa kwa Watanzania kubadilisha fikra zao kuhusu
upatikanaji wa maji, huku wakisisitizwa kuwa uwajibikaji wa uhifadhi wa
rasilimali hii muhimu si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kitaifa,
kisheria, na kimaadili kwa kila raia.
Wachambuzi wa ustawi wa jamii wanasema ili Tanzania ifikie
Dira yake ya Uchumi wa Viwanda ya 2050, wananchi lazima wajione kama 'Walinzi
Namba Moja' wa Rasilimali Maji, wakikubali ukweli wa gharama halisi za maji
safi na kulinda vyanzo kwa ukali.
Dhana potofu ya kwamba maji yanapaswa kuwa bure au
kugharimu kidogo ndiyo inaathiri uwezo wa mashirika ya maji kufanya
matengenezo. Inasisitizwa kuwa maji hugharimu sana katika kusukuma, kutibu kwa
kemikali, na kusambazwa kwa umeme mwingi kutoka vyanzo vya mbali kama Mto Ruvu.
Kama wananchi hawalipii gharama halisi, mashirika hukosa
mapato ya kutosha kufanya ukarabati na kupunguza maji yasiyoingiza mapato
(NRW), na hivyo kuhujumu moja kwa moja uwezo wa Serikali kutoa huduma ya
uhakika.
Aidha wananchi wananchi wanaoishi karibu na vyanzo vya maji
ndio vikosi vya ulinzi vya kwanza. Badala ya kuacha lawama kwa Serikali pekee,
jamii zinapaswa kufanya ufuatiliaji wa kijamii kwa ukali zaidi kuona kwamba
hakuna uharibifu unaofanyika kwenye chanzo au njia ya maji yaani mto.
" Kila mti uliokatwa katika maeneo ya vyanzo huondoa
uwezo wa asili wa ardhi kunyonya mvua. Mtu yeyote anayefanya uharibifu—kama
kukata miti au kilimo kiholela katika maeneo oevu—anapaswa kuonekana kama
mhalifu wa kiuchumi na kuripotiwa mara moja," anasema mmoja wa wachambuzi
hao Said Mmanga.
Katika maeneo kama Dar es Salaam, wananchi wanatakiwa
kuripoti uchimbaji wa visima bila kibali ili kuepusha hatari ya Kuingia kwa
Maji ya Chumvi (Saline Intrusion), ambayo inaweza kuharibu kabisa maji ya
ardhini.
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya wataalamu
wanashauri nchi kuanza kufikiria kusafisha maji ya bahari (Desalination).
Ingawa teknolojia hii ni ghali sana, inatoa uhakika wa maji kwa asilimia 100
dhidi ya ukame, hasa kwa jiji la biashara linalolenga Dira ya 2050. Wananchi
wanapaswa kuijiandaa kisaikolojia kukubali ongezeko la gharama kwa ajili ya
usalama wa maji.
Ulinzi wa maji unahitaji mabadiliko ya utamaduni wa jamii.
Kila Mtanzania, awe anaripoti uvujaji wa bomba au anapanda mti, ni mwekezaji
muhimu katika sekta ya maji, na hivyo kuhakikisha vizazi vijavyo na viwanda
vinapata maji ya kutosha kufikia malengo ya kitaifa.

0 Maoni