Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam
(DAWASA) imetoa taarifa rasmi kuhusu hali ya uzalishaji wa maji, huku
ikitangaza kushuka kwa kiasi kikubwa na kuainisha hatua za kiufundi na
kiutawala zinazochukuliwa ili kurejesha huduma.
Uzalishaji wa maji umeshuka kutoka lita milioni 534.6 kwa
siku hadi lita milioni 270, ikimaanisha upungufu wa lita milioni 264.6 kwa
siku, sawa na karibu asilimia 49.5% ya uzalishaji wa awali. Hali hii imeathiri
wakazi wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani.
Kama ilivyoelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA,
Mhandisi Mkama Bwire, hali imekuwa mbaya zaidi katika Mitambo ya Ruvu. Mtambo
wa Ruvu Chini, wenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 270 kwa siku, kwa sasa
unazalisha takribani lita milioni 50 pekee. Aidha, uzalishaji wa Mtambo wa Ruvu
Juu nao umeshuka kutoka uwezo wake wa lita milioni 196 hadi kufikia lita
milioni 150 kwa siku.
Mhandisi Bwire alibainisha kuwa sababu kuu za upungufu huu
ni athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo mvua za masika kunyesha chini ya
wastani kati ya Machi na Mei, 2025, pamoja na kuchelewa kwa mvua za vuli za
Oktoba hadi Desemba 2025.
Sababu nyingine iliyochangia moja kwa moja ni Mto Ruvu
kubadili mkondo wake wa asili katika eneo la Kitomondo na kutengeneza mchepuko.
Katika kukabiliana na changamoto hii, Bodi ya Maji Bonde la
Wami/Ruvu na DAWASA wanatekeleza mikakati ya muda mfupi na mrefu.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, Mhandisi
Elibariki Mmassy, amesema changamoto ya maji iliyotokea inatokana na athari za
mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri maeneo mengi ya kihuduma.
Kama hatua ya haraka ya kiutawala, Bodi imeendelea na doria
ya kukagua vyanzo vyake vya maji katika mito yote na kusitisha utoaji wa vibali
kwa watumiaji wa skimu za umwagiliaji katika kipindi hiki cha kiangazi kwa
lengo la kuimarisha wingi wa maji. Mhandisi Mmassy alisisitiza kuwa mpaka sasa
hali ya mito iko salama na hakuna uchepushaji mwingine wa maji uliopo.
Kwa upande wa mipango ya muda mrefu, miradi mikubwa kama
vile Bwawa la Kidunda inaendelea kutekelezwa ili kuhakikisha kunakuwepo na
hifadhi ya kutosha ya maji na kupunguza utegemezi wa mtiririko wa mto pekee.
DAWASA imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono
juhudi za serikali za kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa, kwani utulivu
huu ndio msingi wa maendeleo ya Taifa, ikiwemo upatikanaji wa huduma za msingi.

0 Maoni