Serikali ya Tanzania imemfungulia rasmi mashtaka ya uhujumu uchumi ,
Mange Kimambi,Mtanzania anayeishi nchini
Marekani.
Taarifa kutoka kwenye tovuti rasmi ya Mahakama nchini Tanzania zinaonyesha
kuwa kesi hiyo imepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza Alhamisi wiki hii, Desemba
4 na ipo mbele ya Hassan Makube.
Hatua hii ya Serikali inakuja takriban mwezi mmoja baada ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Bw. Hamza Johari, kumlaumu waziwazi mwanaharakati huyo. Bw.
Johari alimtuhumu kuchochea vurugu zilizotokea katika siku ya uchaguzi
uliopita.
Asubuhi ya Desemba 2, 2025, Mange Kimambi mwenyewe alionekana katika
video fupi , akielezea kupokea taarifa za mashtaka hayo akisema anajiandaa.
Jana Rais Samia Suluhu Hassan amesema
waliohamasisha vurugu siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu na siku
zilizofuata walipanga kuangusha Dola, lakini serikali imeapa kuilinda nchi.
“Tunaapa kuilinda nchi hii na mipaka yake, kulinda usalama wa raia na
mali zao, na katika hali hiyo nguvu inayotumika inaendana na tukio lililopo.
Tunapoambiwa kwamba tulitumia nguvu kubwa sana kwenye tukio lile, nguvu ndogo
ilikuwa ni ipi,” Rais Samia alihoji mbele ya wazee hao na viongozi wa serikali.
Aliongeza: “Kuna mengine nasikia yanapangwa, lakini Inshallah Mola
hatosimama nao…litapeperuka.
“Lakini nataka niseme nilimsikia mmoja kati ya waandaaji wa nje anasema
tarehe 9 (siku waliyopanga maandamano) iahirishwe isubiriwe siku ya Krisimasi
sababu sasa hivi tumejipanga…nataka niwaambie wakati wowote wakija
tumejipanga”.
Alisema lililotokea ni tukio la kutengenezwa na waliolitengeneza
walidhamiria kuangusha Dola

0 Maoni