Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, amesisitiza msimamo thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita kulinda amani,
umoja na utulivu wa Taifa, huku akionya dhidi ya matamko yanayoashiria
uchochezi.
Akizungumza kwenye mkutano maalum na Wazee wa Dar es Salaam, Rais Samia
alitoa kauli kali akijibu mfululizo wa matamko yanayotolewa na baadhi ya
taasisi za kidini, hususan Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
“Tupo tayari kukaa, kuzungumza na kuondoa mapungufu yaliyopo, lakini
Serikali hii si ya kuamrishwa wala kupewa maelekezo,” alisema Dkt. Samia.
Rais Samia alifichua kuwa tangu aingie madarakani, TEC imetoa matamko
takribani nane. Hata hivyo, alibainisha kuwa ndani ya Kanisa Katoliki lenyewe
kuna tofauti za kimtazamo kuhusu uhalali na malengo ya baadhi ya kauli hizo.
Alisema baadhi ya viongozi na waumini wa Kanisa wanahoji kuwa matamko
hayo hayajengwi katika misingi ya haki na ukweli, na hivyo kuchochea
migawanyiko isiyo ya lazima katika jamii.
Rais alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia kauli zozote zinazoashiria
uchochezi ama zinazoweza kuvuruga misingi imara ya Taifa.
“Tanzania yetu ni nchi ya umoja, mshikamano, amani na utulivu, na hizo
ndizo ngao zetu. Tusivurugwe ndugu zangu kupitia mirengo ya dini, siasa au
mingineyo,” alihimiza Rais Samia.
Dkt. Samia alieleza masikitiko yake kuwa tuhuma dhidi ya Serikali ya
Awamu ya Sita mara nyingi zimekosa msingi, akitaja mafanikio makubwa katika
sekta mbalimbali.
Aliuliza, "Kosa la Serikali ya awamu ya sita ni nini? Kueneza huduma
bora za afya? Kupeleka elimu bora hadi vijijini? Kukuza uchumi hadi kutambuliwa
duniani? Kuiweka Tanzania salama? Kosa letu ni lipi?"
Alisisitiza kuwa misingi ya kidemokrasia inaruhusu kukosoa, lakini sio
kuhatarisha utulivu wa nchi.
Alitoa wito kwa wananchi kuvumilia na kutokubali vurugu kwa sababu za
tofauti za kidini, asili, au mtazamo binafsi kuhusu kiongozi.
“Kama humpendi anayeongoza, stahimili. Mioyo yetu imeundwa kwa
stahimilivu. Demokrasia ipo, ataongoza na ataondoka. Hakuna sababu ya kuvuruga
nchi,” aliongeza.
Rais Samia alitoa wito mkali kwa viongozi wa dini kutojificha nyuma ya
majoho na kujaribu kuongoza nchi.
Alisema, Tanzania itaendelea
kuongozwa kwa mujibu wa Katiba na sheria, si kwa hisia ama matamanio ya mtu
binafsi.
Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu, lakini
inatarajia taasisi za dini kubaki kuwa chachu ya maadili na sio jukwaa la
mijadala inayoweza kupandikiza migawanyiko.
Rais aliwahimiza wananchi kutumia busara dhidi ya misimamo mikali na
"sumu" wanayopewa, akibainisha kuwa dini mara nyingi hutumiwa
kuwashawishi watu bila uchambuzi wa kina.

0 Maoni