Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa
ufafanuzi wa kina kuhusu vikwazo vya viza vilivyowekwa na Serikali ya Marekani,
ikibainisha kuwa hatua hiyo imetokana na vitendo vya baadhi ya Watanzania
kushindwa kuzingatia sheria za uhamiaji na kugeuza safari za muda kuwa za
kudumu kinyume cha sheria (kuzamia).
Taarifa iliyotolewa leo, Desemba 17, 2025, na Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesisitiza kuwa vikwazo hivyo
si matokeo ya shinikizo la kisiasa au harakati za watu fulani, bali ni matokeo
ya moja kwa moja ya takwimu za uvunjifu wa sheria za viza (Visa Overstays).
Ukweli wa Takwimu: Kwanini Marekani Imechukua Hatua?
Serikali imebainisha kuwa ripoti rasmi za idara ya usalama
wa ndani ya Marekani zinaonyesha kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakikaa nchini
humo muda mrefu zaidi ya ule uliopangwa kisheria. Imeelezwa kuwa Viza za
Matembezi na Biashara (B-1/B-2): Kiwango cha ukiukwaji kimefikia 8.3% wakati
Viza za Masomo na Mashindano (F, M, J): Kiwango cha ukiukwaji ni kikubwa zaidi
kikifikia 13.97%.
"Huu ni ukweli mchungu ambao Watanzania lazima wauone.
Hatua ya Marekani haina uhusiano na kelele za wanaharakati wanaojaribu kujitafutia
sifa mitandaoni. Hili ni suala la kisheria na utaratibu wa nchi. Tunapokwenda
ugenini, ni lazima tuheshimu muda wa kukaa ulioandikwa kwenye viza,"
ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Onyo kwa "Wanaozamia" na Wanaharakati
Serikali imetoa onyo kali kwa watu wanaosafiri kwa
kisingizio cha mambo mbalimbali kisha kutokomea nchini humo kinyume cha sheria.
Vitendo hivyo vinatayarisha mazingira magumu kwa Watanzania wengine wenye
uhitaji wa kweli wa matibabu, masomo, na biashara kupata viza.
Vilevile, Serikali imewataka raia kupuuza madai ya baadhi
ya watu wanaojiita wanaharakati wanaodai kuwa vikwazo hivyo vimetokana na
"harakati" zao. Ukweli ni kwamba nchi nyingine 11 za Afrika, ikiwemo
Nigeria na Zambia, zimepewa masharti hayo hayo kutokana na changamoto kama hiyo
ya raia wao kuzamia.
Hatua za Kidiplomasia
Hata hivyo, Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa tayari
imeshaanza mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Rais Donald Trump ili
kuweka utaratibu utakaowatofautisha wasafiri waaminifu na wale wanaokiuka
sheria, kwa lengo la kuiondoa Tanzania kwenye orodha hiyo.
Wito wa Serikali: "Tanzania ni Taifa imara na lenye
heshima. Watanzania wote wanaokwenda Marekani wanahimizwa kuilinda hadhi ya
nchi kwa kurudi nyumbani pindi muda wao unapoisha. Tusikubali hadhi ya nchi
yetu ichezewe kwa sababu ya maslahi binafsi ya watu wachache wanaotaka kusalia
nchi za watu kinyume cha sheria."

0 Maoni