Dkt. Kijaji ahimiza wananchi kutunza maeneo ya hifadhi

 

Na. Joyce Ndunguru, Njombe

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amewahimiza wananchi wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi ya Mpanga Kipengere kutunza hifadhi hiyo kwa kuzingatia kuwa, takribani vijiji 96 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali na vijiji/miji vya Ilembula, Igawa na Igwachanya vinanufaika na miradi ya maji ambayo chanzo chake ni ndani ya hifadhi ya Mpanga Kipengere.

Mhe. Dkt. Kijaji aliyasema hayo Disemba 17,2025, alipotembelea Hifadhi ya Mpanga Kipengere iliyopo katika Mikoa ya Njombe na Mbeya kwa lengo la kujionea jinsi shughuli za utalii zinavyofanyika, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi katika maeneo yanayosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

“Tusipohifadhi na kuitunza hifadhi yetu hii ya Mpanga kipengere tutakosa maji lakini tutakosa manufaa mengine ya kijamii na kiuchumi tunayopata kupitia hifadhi hii, hivyo niwaombe vijiji vyote vilivyotuzunguka tuweze kuhifadhi kwa pamoja”, alisema Waziri Kijaji.

Sambamba na hilo, Waziri Kijaji aliisisitiza TAWA kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuongeza fursa za uwekezaji na mazao mbalimbali ya utalii katika Hifadhi hiyo.

“Tuje na vivutio vipya vya utalii vilivyomo ndani ya hifadhi yetu , lakini pia tuwaite wawekezaji, tuwauzie fursa ili wawekeze nasi,” aliongeza Waziri Kijaji.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande (Mb) aliwataka watanzania wanaoishi Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo ukanda huu yakiwemo Maporomoko maarufu ya maji ya Kimani yanayopatikana ndani ya Hifadhi ya Mpanga Kipengere.

Naye, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Yussuf Kabange alisema TAWA imeboresha miundombinu mbalimbali ya utalii na utawala iliyopo ndani ya hifadhi ikiwemo ujenzi wa banda za watalii, kambi ya watalii, ofisi, ujenzi madaraja pamoja na barabara.

Kuhusu mahusiano na jamii, Kamishna Kabange alisema vijiji vinavyoizunguka vinanufaika na miradi ya maji ambayo chanzo chake ni ndani ya hifadhi ya Mpanga Kipengere. Aidha, mito iliyopo ndani ya Hifadhi ya Mpanga Kipengere ni vyanzo muhimu vya maji ya skimu za umwagiliaji za Igomelo, Malangali, Wangama, Wangamiko na Imalilo ambazo zinanufaisha jamii moja kwa moja.

Katika ziara hiyo ya kikazi, Waziri Kijaji aliambatana na Naibu Waziri Wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Chande, Naibu Katibu Mkuu (Utalii), Nkoba Mabula na viongozi wengine wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Hifadhi ya Mpanga Kipengere inayopatikana Mikoa ya Njombe na Mbeya ni hifadhi iliyosheheni vivutio vingi likiwemo Maporomoko ya Maji takribani 50 na uwanda uliosheheni maua ya kuvutia.

Chapisha Maoni

0 Maoni