Na. Balozi Mobhare Matinyi
Serikali ya Uswidi tarehe 5 Desemba, baada ya
kupitia vipaumbele vyake vya sera za mambo ya nje na changamoto za kiusalama,
ilitangaza uamuzi wa kufuta misaada yake ya ushirikiano wa maendeleo na nchi
tano kabla ya mwisho wa mwaka 2026, na hivyo kuhitimisha misaada iliyodumu kwa
miongo kadhaa.
Moja ya nchi zilizoathiriwa ni Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, nchi ambayo imedumisha uhusiano mzuri na Uswidi tangia miaka 62
iliyopita. Kufanana katika itikadi ya demokrasia ya kijamii kati ya nchi hizi
mbili ndiko kulikozaa uhusiano huu wa kipekee. Waumini wa demokrasia ya kijamii
huamini katika haki ya kijamii, uhuru, usawa, utu wa binadamu na mshikamano
ndani ya mfumo wa demokrasia unaoruhusu serikali kuingilia ubepari ili
kuwezesha ustawi wa jamii.
Hata hivyo, wakati Uswidi ikiwa na demokrasia ya
vyama vingi na kujali ustawi katikati ya ubepari, Tanzania ilichagua kufuata
mfumo wa demokrasia ya chama kimoja kinachofuata Ujamaa wa Kiafrika ambayo
ilisisitiza kujitegemea. Uswidi hivyo basi, ikachukua jukumu la kuwa mkufunzi
wa harakati za vyama vya ushirika kwa Tanzania wakati huo.
Nchi hizo mbili zilikuwa zikitofautiana katika
maendeleo ya kiuchumi kwa kiasi kikubwa kwani Uswidi iliyokuwa na watu milioni
7.5, ilikuwa na Pato la Taifa la dola za Marekani bilioni 17.33 mwaka 1961,
huku ikiendesha uchumi imara wa viwanda wakati Tanzania iliyokuwa na watu
milioni 10.3 ilikuwa na Pato la Taifa la dola za Marekani bilioni 2.83 huku
ikitegemea zaidi uchumi wa kilimo.
Kwa hiyo Uswidi, mwaka 1963, iliona umuhimu wa
kuiunga mkono Tanzania, wakati huo Tanganyika kabla ya kuungana na Zanzibar mwaka
1964 na kuunda Tanzania, kwa sababu nchi hiyo mpya ilikuwa imeonyesha dira
makini ya maendeleo chini ya Rais Julius Nyerere.
Tangazo la hivi majuzi la Serikali ya Uswidi, bila
kukusudia, liliibua simulizi iliyoipotosha taswira ya Tanzania na mafanikio
yote ya ushirikiano huu wa fahari. Ilidaiwa kuwa nchi zilizotajwa
"zimekuwa zikifuata Ujamaa mno" kwa miongo mingi na matokeo yake
"hazijaendelea".
Niseme wazi vizuri kabisa: Kauli hiyo haiendani na
Tanzania kwa namna yoyote ile, hata kwa fikra tu.
Hebu tuangalie ukweli: Mwanzoni mwa miaka ya 1960
Tanzania ilikuwa na chuo kikuu kishiriki kimoja tu, lakini leo ina vyuo vikuu
36 vilivyosajiliwa na vyuo vikuu vishiriki 16. Uswidi, kwa upande wake, leo ina
vyuo vikuu 18 vilivyosajiliwa na vyuo vikuu vishiriki 12. Kwa hakika, ikiwa na
takribani watu milioni 70, Tanzania bado inahitaji vyuo vikuu zaidi
ikilinganishwa na Uswidi yenye milioni 10.7.
Wakati huo Tanzania ilikuwa na vituo kutolea huduma
za afya 1,343 zikiwemo hospitali 96 na vituo vya afya 22. Leo Tanzania ina
vituo vya aina zote vya kutolea huduma za afya 13,606 zikiwemo hospitali 473 na
vituo vya afya 1,348. Tunashukuru kwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Chuo
Kikuu cha Karolinska ya jijini Stockholm na Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyo
pamoja na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili.
Tanzania ilianza na uwanja wa ndege wa kimataifa
mmoja jijini Dar es Salaam lakini imeongeza viwanja viwili Kilimanjaro na
Zanzibar na vingine viwili Dodoma na Mwanza vikiendelea kujengwa. Nayo Uswidi
ina viwanja vya ndege vya kimataifa vikubwa zaidi huko Stockholm, Gothenburg na
kidogo cha Malmo.
Ikiwa katika ukanda wa kimkakati wa mwambao wa
Afrika Mashariki, Tanzania inahudumia nchi kadhaa zisizo na bandari kupitia
bandari zake kuu nne za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na Zanzibar, na hivi
karibuni itaanza ujenzi wa bandari kubwa ya Bagamoyo. Pia kuna bandari kadhaa
kwenye maziwa makuu matatu ya Afrika, Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Mtandao mkubwa wa barabara na reli wa Tanzania ni
miongoni mwa mitandao yenye ufanisi mkubwa barani Afrika na unaendelea kukua.
Tunaipongeza Serikali ya Uswidi kwa kuunga mkono kwa njia mbalimbali mradi wetu
wa reli ya kisasa (SGR), reli ya kwanza inayotumia umeme Afrika Mashariki na
Kati. Kwa sasa reli hiyo inafanya kazi kati ya Dar es Salaam na mji mkuu
Dodoma. Miradi zaidi ya reli katika maeneo ya kaskazini na kusini mwa nchi,
ambayo kimsingi itaunganisha nchi zaidi na bahari ya Hindi, iko mbioni.
Baada ya miaka michache, Tanzania itakuwa kitovu
kikubwa cha nishati baada ya kukamilisha mradi wa gesi asilia na kampuni ya
Norway, Equinor, wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 42. Aidha, mradi wa
Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki linaloanzia Uganda hadi bandari ya
Tanga unakaribia kukamilika.
Vilevile, Tanzania, ambayo inazalisha maelfu ya
megawati za umeme kwa kutumia mitambo ya nguvu za maji, imejiandaa vizuri
kutumia vyanzo vingine vya nishati mbadala kama jotoardhi, upepo na jua.
Kadhalika, Tanzania ina akiba kubwa ya makaa ya mawe inayokadiriwa kufikia tani
bilioni 1.9.
Mtazamo wa uchumi wa Tanzania pia ni wa kuvutia.
Ingawa Pato lake la Taifa linakaribia dola bilioni 90, ukuaji wa uchumi kama
inavyoshuhudiwa na Benki ya Dunia na Shirika la Mikopo ya Mauzo ya Nje la
Uswidi (EKN) umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 5-7 kila mwaka tangu mwaka
2000. Nchi zingine zenye uchumi imara kama Uswidi, yenye Pato la Taifa la dola
bilioni 630, imepata ukuaji hasi mara mbili ndani ya miaka mitano iliyopita.
Mnamo Julai 2020, Tanzania ilihitimu kutoka nchi za
kipato cha chini na kuingia kwenye kundi la nchi za kipato cha kati, ambayo kwa
mujibu wa Benki ya Dunia inaashiria maendeleo makubwa ya uchumi na utulivu kwa
miongo miwili. Haya ni matunda ya mageuzi ya mwanzoni mwa miaka ya 1990 ambayo
yaliipeleka nchi katika uchumi mchanganyiko, na mfumo wa demokrasia ya vyama
vingi vya siasa, mchakato unaohitaji miongo kadhaa kukomaa.
Tanzania ilipokea korona za Uswidi milioni 560 mwaka
2024, takriban dola milioni 60 za Marekani, kama msaada kutoka Uswidi. Lakini
Tanzania sasa inahama kutoka kwenye misaada kwenda kwenye biashara na
uwekezaji; hivyo, inakaribisha wawekezaji wa Uswidi katika sekta muhimu kama
viwanda, huduma, madini, utalii, kilimo na teknolojia.
Ni dhahiri kuwa, katika mwaka unaoishia Septemba
2025, Tanzania ilikusanya dola bilioni 4.43 kutokana na dhahabu, bidhaa
inayoongoza kwa mauzo ya nje nchi, huku ikitarajia utalii utaleta dola bilioni
6.0 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2025. Tanzania kwa sasa ndiyo nchi inayoongoza
duniani kwa utalii wa mbugani kwa mwaka wa tatu mfululizo, ikijivunia Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na fuko
maridadi za Zanzibar.
Tanzania ina hifadhi kubwa ya madini muhimu ikishika
nafasi ya tatu barani Afrika na ya sita duniani. Ufini inatusaidia katika
utafutaji na utafiti wa utajiri huu wa kipekee, ambao kwa hakika utainua uchumi
wetu. Uswidi inahimizwa kutumia fursa za kujenga mitambo ya kuchenjua madini
nchini.
Mwaka 2024 pekee, Tanzania ilivutia uwekezaji wa
moja kwa moja wenye thamani ya dola bilioni 9.31 kutokana na miradi 901
iliyosajiliwa, na nchi hii inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 140.
Pamoja na mafanikio haya, serikali ya sasa chini ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mikakati zaidi ili kuwaletea
Watanzania maendeleo thabiti na endelevu.
Hivyo basi, kwa dhati kabisa, kwa uchumi wenye sekta
nyingi na unaofuata soko huria huku ukionesha ukuaji stahimilivu wa kuvutia,
kuibagaza Tanzania kwamba "imelowea kwenye Ujamaa usio na maendeleo"
si sahihi na ni upotoshaji.
Mwandishi ni Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika nchi za Nordic, Baltic na Ukraine, mwenye
makazi yake Stockholm.

0 Maoni