Na
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, amesema Serikali ya
Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha ushirikiano na waandishi wa habari wa
mitandaoni na mabloga kwa lengo la kujenga tasnia ya habari iliyo imara, yenye
weledi na inayolinda maslahi ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam, Ndg. Msigwa alisema serikali imechagua mkondo wa kushirikiana na
kuwalea wadau wa habari badala ya kuchukua hatua za adhabu, akibainisha kuwa
mitandao ya kijamii imekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano ya kisasa na ujenzi wa
taifa.
Alieleza kuwa katika dunia ya sasa, mapambano mengi
yamehama kutoka uwanja wa kijeshi kwenda kwenye uwanja wa taarifa, hali
inayofanya kazi ya waandishi wa habari kuwa nyeti kwa mustakabali wa nchi.
“Habari mnazozitoa zinaweza kuijenga nchi au
kuharibu taswira yake. Ndiyo maana serikali inaona umuhimu wa kushirikiana
nanyi,” alisema Msigwa.
Ndg. Msigwa aliipongeza Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) kwa mwelekeo wake wa kulea wadau wa sekta ya habari, akisema
hatua hiyo imeongeza imani kati ya serikali na waandishi wa habari wa
mitandaoni. Pia aliitaja TBN na JUMIKITA kuwa ni wadau wakubwa wa serikali
katika kusambaza taarifa sahihi kwa umma.
Katibu Mkuu huyo aliwahakikishia waandishi wa habari
ulinzi wa serikali, akieleza kuwa endapo sheria, kanuni au sera zitabainika
kuwa kikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao, serikali iko tayari kuzifanyia
marekebisho kwa maslahi mapana ya taifa.
Aidha, alisema serikali kwa kushirikiana na TCRA na
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo katika maandalizi ya kutoa
mafunzo maalum kwa waandishi wa habari wa mitandaoni, pamoja na kuandaa
mikakati ya kuwawezesha kiuchumi.
Kuhusu masuala ya kodi, Ndg. Msigwa alisema serikali
itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kutatua
changamoto zinazowakabili waandishi wa habari wa mitandaoni, huku ikitambua
mchango wao mkubwa katika kuitangaza Tanzania na kuvutia wawekezaji.
Akihitimisha, Ndg. Msigwa aliwataka waandishi wa
habari kutumia majukwaa yao kwa uzalendo, uwajibikaji na weledi, akisisitiza
kuwa serikali inawaona kama washirika muhimu katika ujenzi wa taifa na
kuimarisha demokrasia.



0 Maoni