Kampeni kubwa ya
kukataa maandamano yanayolenga kuvuruga amani na utulivu wa nchi imechukua
kasi, huku sauti za vijana, hasa mabinti, zikiibuka kwa nguvu kupinga vitendo
hivyo. Wakizungumza kwa umoja, wametoa wito kwa vijana wenzao kuacha kutumiwa
na watu wenye maslahi binafsi na badala yake waendelee kulinda amani
waliyozaliwa nayo.
Akizungumza na
waandishi wa habari jijini Dodoma
Alhamisi Desemba 4, 2025, Bi. Beatrice Mwahegili, Katibu Msaidizi wa Idara
ya Mabinti na Uwezeshaji wa Taasisi ya Mama Asemewe, alisisitiza kuwa hakuna
Tanzania nyingine na gharama ya kurejesha amani pale itakapopotea ni kubwa mno.
"Tunapinga
vikali maandamano yanayoendelea kuhamasishwa tarehe 09. Tarehe tisa ni siku
ambayo Taifa letu lilipata uhuru, si siku ya vurugu au kuhamasisha machafuko
katika Tanzania yetu," alisema Bi. Beatrice huku akisisitiza wajibu wa
kwanza wa vijana kuitunza amani.
Ameongeza kwa
kuwataka vijana "kuamka na kutokubali kutumika kwa maslahi ya watu
wachache," na kuwakataa wale wote wanaohamasisha vitendo vya uvunjifu wa
amani nchini.
Mwahegili
alibainisha wazi kuwa amani iliyopo ndio msingi wa maendeleo na ustawi wa
mabinti, vijana, na jamii nzima ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa
fursa lukuki za kiuchumi.
"Kipindi cha
Rais Samia ametugusa mabinti kwa asilimia kubwa sana," alisisitiza
kiongozi huyo wa vijana, akieleza jinsi fursa hizi zinavyowapa vijana
kipaumbele na kuwaondoa katika hatari ya kutumiwa kisiasa.
Katika muktadha
huu, Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa mwelekeo wa jinsi serikali
ilivyojiandaa kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kutishia amani.
Akihutubia taifa hivi karibuni, Rais Samia alisisitiza kuwa jukumu la kwanza la
serikali ni kulinda usalama wa raia na mali zao.
Rais alieleza kuwa
serikali ina mipango imara ya kuhakikisha utulivu unaendelea, akibainisha kuwa
uhuru wa kukusanyika na kutoa maoni unapaswa kuheshimu sheria na kanuni
zilizopo nchini.
"Hatutakubali
mikakati yoyote ile itakayolenga kurudisha nyuma maendeleo yetu tuliyoyapata
kwa jasho na damu. Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimeelekezwa kuchukua hatua
stahiki kwa mujibu wa sheria dhidi ya yeyote atakayejaribu kuvuruga amani
yetu," alisema Rais Samia.
Kauli hiyo ya Rais
inaakisi maandalizi ya serikali ya kisheria na kiulinzi, huku ikituma ujumbe
wazi kwamba wakati serikali iko tayari kusikiliza maoni, haitavumilia vitendo
vinavyohatarisha usalama wa Taifa.

0 Maoni