Kwa mara ya kwanza Taasisi ya Moyo
Jakaya Kikwete (JKCI) yawekea historia Tanzania, Afrika Mashariki na Kati kwa
kutoa matibabu mapya ya tiba ya kupunguza msisimko wa shinikizo la damu katika
mishipa ya figo (Renal denervation therapy).
Matibabu hayo ambayo yameanza kutolewa
leo katika Taasisi hiyo yanatolewa kwa wagonjwa wenye matatizo ya shinikizo la
juu la damu la muda mrefu ambalo halishuki kwa matibabu ya dawa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini
Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.
Peter Kisenge alisema yatizo la shinikizo la juu la damu huchangia kwa asilima
25 ya magonjwa yote yasiyoambukiza hivyo kupelekea vifo vingi vya ghafla na
kuongeza idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji huduma ya kusafishwa damu
(dialysis).
"Matibabu haya hutibiwa kwa
kutumia mashine ya radio frequency ultrasound ambayo inaenda kuchoma mishipa
inayoenda kwenye figo ili kuweza kupunguza tatizo la shinikizo la juu la damu
na kuwa la dawaida", alisema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema kupitia matibabu
hayo wagonjwa wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu la muda mrefu
wanapunguziwa hatari ya kupata kiharusi, magonjwa ya figo kutofanya kazi vizuri
lakini pia inasaidia kudhibiti uzalishaji wa homoni zinazopandisha shinikizo la
damu.
"Matibabu haya ni ya gharama
sana, mgonjwa mmoja inaweza mgharimu kiasi cha shilingi milioni 22 kupata
huduma hii lakini kupitia Serikali yetu wagonjwa wanaopata huduma hii leo
watatibiwa kwa kuchangia kidogo na wale wasiokuwa na uwezo watatibiwa bila
gharama", alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa
magonjwa ya moyo kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri Prof. Mohamed
Atef alisema matibabu hayo yanatoa matumaini kwa wagonjwa wenye matatizo ya
shinikizo la damu la juu ambao wamekuwa wakitumia dawa kwa muda mrefu bila ya
mafanikio.
"Leo tutawapatia matibabu
wagonjwa sita hadi saba wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu la muda
mrefu kwa kufanyiwa upasuaji mdogo kupitia tundu dogo lililopo kwenye paja na
kuunguza mishipa ya damu inayoelekea kwenye figo na kusababisha matatizo ya
figo", alisema Dkt. Atef.
Dkt. Atef alisema Tanzania inapaswa
kujivunia kwa kuwa na Taasisi ya Moyo nchini ambayo inatoa matibabu ya kibingwa
ya magonjwa ya moyo na kuongeza ujuzi katika kutoa matibabu hayo.
"Ninafura kwa kuwa daktari
wakwaza kufikisha ujuzi huu hapa JKCI, naupongeza sana uongozi wa hapa kwa
kuhakikisha ndoto ya kufikisha matibabu bingwa na mbinu mpya kwa wagonjwa wake
inatimia", alisema Dkt. Atef.
Naye mgonjwa aliyekuwa akisubiri
kupatiwa matibabu hayo Donasian Meleki aliushukuru uongozi wa JKCI kwa
kumruhusu kuchangia kidogo matibabu hayo na gharama zilizobaki kulipwa na
Serikali.
Meleki alisema ugonjwa wa shinikizo la
damu amekuwa nao tangu mwaka 2011 ambao umemsababishia kupata matatizo ya figo
na kufikia hatua ya kusafisha damu (dialysis).
"Naishukuru Serikali ya Tanzania
kwa kujali afya za watu wake, hapa ndio naenda kufanyiwa upasuaji ninaimani
nitatoka salama na kupunguza matatizo yaliyopo katika mwili wangu hivyo
kuendelea kulitumikia Taifa", alisema Meleki.
Matibabu ya tiba ya kupunguza msisimko
wa shinikizo la damu katika mishipa ya figo (Renal denervation therapy)
yalianza kutolewa duniani mwaka 2013 lakini hayakuwa na mafanikio mazuri hivyo
kufanyiwa utafiti ambao sasa umeonesha mafaniko na kuanza kutolewa tena kwa
wagonjwa wenye matatizo ya shinikizo la juu la damu la muda mrefu ambalo
halishuki kwa kutumia dawa.

0 Maoni