Kuelekea maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi, Mchungaji
mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja,
ametoa wito mzito kwa Watanzania akisisitiza kuwa sikukuu hii ni mahususi kwa
ajili ya kumtukuza Mungu na kuhubiri amani, na si jukwaa la harakati za
kisiasa.
Mchungaji Hananja ameeleza kuwa jaribio lolote la kuingiza
uanaharakati au maandamano ndani ya misingi ya kidini wakati wa msimu huu wa
sikukuu ni sawa na kufuru. Akirejea maandiko matakatifu, amekumbusha kuwa
ujumbe wa kwanza wa kuzaliwa kwa Yesu Kristo ulikuwa ni amani kwa wanadamu.
"Krismasi ni sikukuu ya kumtukuza Mungu. Malaika
walitangaza amani, na Luka 2:12 inatupa ishara ya mwokozi aliyeleta amani
duniani. Kugeuza madhabahu au siku hii kuwa sehemu ya harakati ni kwenda
kinyume na mapenzi ya Mungu," alisema Mchungaji Hananja.
Kauli hiyo ya Mchungaji imeungwa mkono na sehemu kubwa ya
wananchi ambao wamejitokeza kusisitiza umuhimu wa utulivu. Kupitia mijadala
mbalimbali, wananchi wameonya dhidi ya vikundi vinavyojaribu kuchochea
machafuko au maandamano wakati wa msimu wa sikukuu.
Wananchi wamehimiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na
mshikamano wa kitaifa ni tunu inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote.
Kutokana na msimamo huo
wananchi wamekuwa mtandaoni
wakionesha msimamo dhidi ya maandamano kwa kauli mbiu za
#Hatuandamani huku wengi wakisema kuwa wanaochochea vurugu wana ajenda za siri
ambazo hazina maslahi kwa Taifa.
Wananchi wametoa tahadhari kwa vijana kutokubali kutumiwa
na watu "waliohongwa" ili kuharibu utulivu wa nchi.
Mchungaji Hananja amewataka Watanzania kusherehekea kwa
furaha na utulivu majumbani mwao na katika nyumba za ibada, akisisitiza kuwa
amani ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yoyote.

0 Maoni