Mwandishi Wetu Endulen Ngorongoro
Uhusiano kati ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
(NCAA) na jamii inayoishi ndani ya eneo la hifadhi umeendelea kuimarika
kufuatia ziara za Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Bw. Abdul-Razaq Badru katika
vijiji mbalimbali vilivyoko tarafa ya Ngorongoro ambapo leo tarehe 20 Desemba, 2025
ametembelea Kata ya Enduleni, wilayani Ngorongoro.
Akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa
Menejimenti ya Ngorongoro na Diwani wa Kata ya Endulen Mhe. Elias Sakara Nagol,
Kamishna Badru ameeleza kuwa, lengo la ziara hiyo ni kuendelea kuimarisha
uhusiano kati ya Uongozi wa hifadhi ya Ngorongoro na jamii, pamoja na kukagua
maboresho ya miundombinu ya maji inayotumika kwa matumizi ya wananchi, mifugo na wanyamapori.
Katika ziara hiyo Kamishna Badru amewaeleza wananchi
wa vijiji vya Kata ya Enduleni kuwa Mamlaka inatekeleza Miradi ya Maji katika
kata za Endulen, Kakesio, Olbalbal na maeneo mengine na aliwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu
katika usimamizi na utunzaji wa miradi hiyo ambayo inagharimu fedha za
Serikali.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Enduleni, Dkt.
Elias Sakara Nagol, amempongeza Kamishna Badru na wasaidizi wake kwa kuendeleza
uhusiano ya karibu na jamii inayoishi
ndani kwa kuwatembelea mara kwa mara,
kusikiliza kero zao na kushirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kijamii na
kuahidi kuwa wananchi wataendelea kuwa mabalozi wazuri wa kutunza na kulinda
hifadhi kupitia programu ya uhifadhi shirikishi.




0 Maoni