Katika ulimwengu wa sasa ambapo teknolojia ya mawasiliano imekua kwa kasi, simu janja mkononi mwa kijana imekuwa silaha yenye nguvu inayoweza kujenga mustakabali wa nchi au kubomoa misingi ya amani iliyodumu kwa miongo mingi.
Wakati
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikihimiza uhuru wa kutoa maoni kama
haki ya kikatiba, kumeibuka changamoto ya baadhi ya vijana kutumbukia kwenye
makosa ya jinai kupitia mitandao ya kijamii, ama kwa kufuata mikumbo ya kisiasa
au kwa kukosa uelewa wa mipaka ya kisheria.
Ili
kulinda usalama wa taifa na mustakabali wa vijana wenyewe, kuna haja ya kuwa na
uelewa wa kina juu ya maadili ya kidijitali yanayozingatia uzalendo na utii wa
sheria.
Msingi
wa kwanza wa kuwa raia mwema wa kidijitali unaanza na dhana ya kuhakiki taarifa
kabla ya kuzisambaza. Katika mazingira ya sasa ambapo taarifa za uongo au
"Fake News" husambaa kwa kasi ya ajabu, ni wajibu wa kila kijana
kujiuliza juu ya ukweli wa jambo kabla ya kubofya kitufe cha kusambaza.
Sheria
ya Makosa ya Mtandao iko wazi kuwa kusambaza taarifa ambazo mtu anajua au
anapaswa kujua kuwa ni za uongo na zinaweza kuleta taharuki nchini ni kosa la
jinai. Badala ya kuwa sehemu ya kusambaza uzushi kuhusu usalama wa taifa au
afya za viongozi, kijana mzalendo anapaswa kusubiri taarifa kutoka kwenye
vyanzo rasmi vya serikali na vyombo vya habari vinavyotambulika.
Hali
kadhalika, kuna tofauti kubwa kisheria kati ya kukosoa utendaji wa serikali na
kutoa lugha za kashfa au kejeli dhidi ya viongozi na mamlaka halali. Kukosoa
sera au mipango ya maendeleo kwa lengo la kuleta maboresho ni sehemu ya ujenzi
wa taifa na ni haki inayolindwa. Hata hivyo, kutumia lugha za matusi,
kudhalilisha utu wa mtu, au kutoa lugha za kashfa dhidi ya Rais na viongozi
wengine ni ukiukwaji wa maadili na uvunjifu wa sheria. Kijana anayejitambua
anapaswa kujikita kwenye hoja zenye mashiko (issues) na siyo kushambulia watu
binafsi, kwani kufanya hivyo kunapunguza uzito wa hoja na kumfanya mdau wa
mtandao kuonekana kama mchochezi badala ya mjenzi wa hoja.
Uzalendo
wa kidijitali pia unadai kukataa katakata matumizi ya mitandao kupandikiza
chuki za kidini, kikabila, au kisiasa zinazolenga kuwagawa Watanzania. Kauli
zinazohamasisha watu kuasi mamlaka halali au kuingia mitaani kufanya vurugu,
kama zile zinazojaribu kushawishi vijana wasishiriki katika sherehe za kitaifa
au kususia shughuli za maendeleo, ni uchochezi unaopaswa kupingwa.
Amani
ya nchi ndiyo inayowezesha mitandao hiyo kuwepo na kutumika; bila amani, hakuna
jukwaa la kidijitali litakalokuwa salama. Ni wajibu wa kila kijana kutumia
sauti yake mtandaoni kuzungumzia "Mazao ya Amani" kama vile fursa za
kiuchumi, miradi ya kimkakati, na umoja wa kitaifa badala ya kugeuka chombo cha
mabeberu na wachochezi.
Mwisho,
vijana wanapaswa kutambua kuwa kila kitu wanachokiweka mtandaoni leo
kinatengeneza historia yao ya kidijitali ambayo inaweza kuwasaidia au kuwaponza
hapo baadaye.
Badala
ya kutumia mitandao kama shimo la kulalamika na kutoa lawama zisizoisha, ni
wakati wa kuitumia kama jukwaa la kibiashara, kuinadi miradi ya kijamii, na
kutafuta fursa za kiuchumi zinazotangazwa na serikali kupitia wizara
mbalimbali. Viongozi kama Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na wengine wamekuwa
wakisisitiza umuhimu wa vijana kuchangamkia fursa za mikopo na mitaji. Kijana
mjanja ni yule anayetumia simu yake kutengeneza andiko la mradi na
kuliwakilisha kwa mamlaka husika, badala ya kutumia muda mwingi kusikiliza
miradi ya vurugu ya watu wachache wenye nia ya kuivuruga Tanzania kwa maslahi
yao binafsi.

0 Maoni