Imesisitizwa kuwa amani ya Tanzania ni tunu ya kipekee
ambayo ni lazima ilindwe na kila mwananchi kwa wivu mkubwa, kwani ndiyo msingi
mkuu unaomwezesha kila mtu kutimiza wajibu wake na kupata haki zake za msingi.
Katika mazungumzo maalumu kupitia kipindi cha #DAKIKA45
ndani ya ITV, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, amebainisha kuwa bila amani,
hakuna maendeleo wala utulivu wa kijamii unaoweza kupatikana.
"Amani ni msingi; palipo na amani unajua wapi pa
kuzitafuta haki zako na utatimiza wajibu wako. Tunahitaji amani ili mifumo ya
maisha na taasisi za kutoa haki ziweze kufanya kazi vizuri," alieleza
Wakili Mpanju.
Matumizi Mabaya ya Mitandao
Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka kundi dogo la watu
wanaotumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kusambaza lugha za uchochezi na
kukejeli juhudi za kulinda utulivu wa nchi.
Katika maoni mtandaoni yaliyoambatana na kauli ya Naibu
Katibu mkuu huyo imesisistizwa uzalendo wa kidijitali ambapo Kila Mtanzania
anapaswa kutumia mitandao ya kijamii kujenga nchi na si kuibomoa. Aidha
imeelezwa kuwa ni muhimu kupuuza na kuripoti maudhui yoyote yanayolenga
kupandikiza chuki au hofu miongoni mwa jamii.
Pia inapaswa itambuliwe kwamba amani yetu haikuja kwa bahati
mbaya; imejengwa kwa misingi ya umoja na mapatano. Watu wanaojaribu kuchezea
amani hii wanapaswa kutambuliwa kama maadui wa maendeleo ya kila mwananchi.
Aidha ni jukumu la kila mdau wa amani kuhakikisha kuwa
Tanzania inabaki kuwa kisiwa cha utulivu. Hii ni pamoja na kusaidia mamlaka
kuwafichua wale wote wanaopanga njama za kuvuruga usalama wa nchi kupitia
majukwaa ya kiteknolojia.
Tanzania ni Taifa Teule
Wadau mbalimbali wameendelea kupongeza juhudi za Serikali
katika kuhakikisha amani inatawala. Wananchi wamehimizwa kuendelea kuwa wamoja,
kushirikiana, na kuombea Taifa ili njama zozote za kuichafua Tanzania
zisifanikiwe.
Amani inapotawala, kila mwananchi kuanzia ngazi ya familia
hadi Taifa anapata fursa ya kustawi kiuchumi na kijamii. Ni wajibu wetu sote
kuilinda Tanzania yetu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

0 Maoni