Taswira ya amani na utulivu imetawala katika mji wa mpakani
wa Tunduma, mkoani Songwe, baada ya zaidi ya vijana 600 wa kabila la Wasafwa
kufanya matembezi makubwa ya kitamaduni yaliyopambwa na nyimbo, ngoma, na
shamrashamra za kipekee.
Tukio hilo lililofanyika Desemba 2025, limekuwa kielelezo
tosha kuwa amani ndiyo msingi wa furaha. Bila utulivu uliopo nchini,
isingewezekana kwa kundi kubwa la vijana kukusanyika, kufunga barabara kwa muda
kwa amani, na kuonesha utajiri wa asili yao bila hofu yoyote.
Baraka Thomson
Mwashobezya, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Kisafwa Tunduma amesema
maandamano yao ya amani ya kuenzi utamaduni na ushirikiano yamewezekana
kutokana na amani iliyopo na kusihi vijana wenzake kutambua umuhimu wa amani
katika maisha na katika shughuki zao za kujiletea maendeleo.
Alisema umoja huo wenye wanachama zaidi ya 600 umeundwa
kuhamasisha kujitambua na kushikamana, kukosoana na kusaidiana ili vijana
wasonge mbele kimaendelkeo na kijamiii.
Ujumbe wa Amani na Kazi
Maadhimisho hayo ya kutimiza mwaka mmoja wa umoja wa vijana
hao yamebeba jumbe nzito zenye mwelekeo wa kijamii na kiuchumi:
Dawa ya Umasikini ni Kazi
Moja ya kauli mbiu zilizovuma katika tukio hilo ni
"Idawa yi yipina wawombe mbombo", ikiwa na maana ya kuhimiza vijana
kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi, jambo ambalo linawezekana tu
palipo na utulivu.
Kuenzi Utamaduni
Vijana hao wameonesha kuwa amani inatoa fursa kwa vizazi
vipya kujivunia lugha na asili yao. Hii inajenga utambulisho wa Taifa na kuzuia
mmomonyoko wa maadili.
Mshikamano wa Makabila
Licha ya kuwa ni sherehe ya Wasafwa, wadau kutoka makabila
mengine kama Wanyakyusa wameonekana kuunga mkono na kufurahia ngoma hizo, jambo
linalothibitisha kuwa Tanzania ni nchi ya umoja na mapatano.
Tusiharibu Amani Yetu
Wachambuzi wa masuala ya kijamii wanabainisha kuwa matukio
kama haya ya Tunduma ni ukumbusho kwa kila Mtanzania kuwa amani ni tunu
isiyopaswa kuchezewa.
"Tunapata fursa ya kucheza, kuimba, na kusherehekea
umoja wetu kwa sababu nchi iko salama. Tukiharibu amani, hata hizi ngoma za
asili na furaha tuliyonayo leo vitatoweka," alisema mmoja wa waandaaji wa
matembezi hayo.
Maoni ya Wananchi
Mitandao ya kijamii imelipuka kwa furaha huku watu wengi
wakipongeza hatua hiyo ya vijana wa Kisafwa. Wengi wamesisitiza kuwa kuona
vijana wanajivunia asili yao (Wasafwa Hoyeee!) ni ishara ya taifa
linalojitambua na linaloishi kwa upendo.
Tukio la Tunduma ni somo kuwa amani si neno tu, bali ni
mazingira yanayoruhusu utamaduni kunawiri, vijana kufanya kazi, na jamii kuwa
na furaha. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa chokochoko za aina
yoyote hazivurugi uzuri huu wa Kitanzania.

0 Maoni