Mfanyabiashara na mwanamitandao maarufu nchini, Niffer,
amewajia juu watu wanaochukua video zake, kuzihariri (editing), na kuziposti
kwenye kurasa zao kwa lengo la kupotosha maana na kumchonganisha na wateja wake
au na serikali.
Katika video yenye sauti kali aliyoiposti hivi karibuni,
Niffer ameonekana kutofurahishwa na tabia ya baadhi ya watu wanaotumia jina
lake kwa manufaa yao binafsi, huku wakiharibu taswira ya biashara zake ambazo
amezitolea jasho.
"Mmetumwa na Nani?"
Niffer amewahoji wanaofanya vitendo hivyo kama kuna watu
wanawalipa fedha ili kumharibia, akisisitiza kuwa hataki "shobo" na
mtu yeyote na anataka aachiwe afanye biashara zake kwa amani.
"Unaposti page yangu wewe kama nani? Wewe ni nani
kwangu? Kama unataka kunisapoti, nisapoti katika biashara kwa kuposti video
yote, lakini siyo kuposti upotoshaji. Mmetumwa nini?" alihoji Niffer kwa
ukali.
Akaunti Kufungwa: "Sikio la Kufa Halisikii Dawa"
Niffer amethibitisha kuwa tayari baadhi ya watu
wameshapoteza akaunti zao baada ya kuripotiwa , na amewatahadharisha wengine
kuwa zoezi hilo linaendelea kama hawataacha kutumia video zake vibaya.
"Jana niliposti nikasema; kama umechukua video yangu
ukaenda kuposti kwenye udaku au kupotosha maana ya kile nilichoposti, mtapoteza
hizo hizo akaunti. Kuna mdada ana kisebengo na mkaka yuko huko... mjifunze
kuheshimu majina ya watu. Mimi siyo mjinga."
Fundisho la "Ndani": Niffer Siyo Yule wa Zamani
Akikumbushia kipindi alichopata changamoto za kisheria na
"kuingia ndani" (mahabusu), Niffer amesema alichojifunza huko
kinatosha na kwamba hataachia mtu yeyote achezee jina lake kwa manufaa ya
udaku.
"Nilichojifunza kule (ndani) ni kuwa nisitegemee mtu
atumie jina langu kwa manufaa yake binafsi. Stress tulizopata mwanzo
zimeshatutosha. Ukichukua video yangu ukaenda kuweka maana nyingine,
tutafikishana pabaya."
Ujumbe kwa Wateja na Mashabiki
Niffer ameweka wazi kuwa ana wateja (customers) na watu
wanaomtazama kama mfano (role models), hivyo hataki maudhui yanayokatisha watu
tamaa ya kufanya kazi. Amesema wakati akiwa kwenye matatizo, wateja wake
walimfariji, lakini "wambea" hawakuwepo.
"Niacheni na biashara zangu. Hii serikali isingekuwa
inaniamini isingenifungulia nifanye biashara. Mnaumia nini mimi kuwepo uraiani?
... mchuma janga hula na wa kwao."
Habari hii imepokelewa kwa hisia mseto mitandaoni, huku
wafanyabiashara wenzake wakimpongeza kwa kulinda "brand" yake, huku
wapenda udaku wakionywa kukaa mbali na maudhui ya mwanadada huyo ambaye kwa
sasa hana mzaha kwenye biashara.

0 Maoni