Madagascar yaachia madaraka SADC, Samia , Mutharika, Hermie wapongezwa

 

Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamepongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuchaguliwa kwake katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 2025.

Aidha wakuu hao pia waliwapongeza viongozi wengine waliochaguliwa katika chaguzi zilizofanyika kati ya Septemba na Oktoba 2025 ambao ni Rais wa Malawi, Prof. Arthur Peter Mutharika, na Rais wa Seychelles, Dkt. Patrick Herminie.

Pongezi hizo zimetolewa katika  Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi na Serikali (Extraordinary Summit) uliofanyika kwa njia ya mtandao Novemba 7, 2025, ambapo viongozi hao walijadili masuala muhimu ya kikanda.

Pamoja na pongezi Mkutano huo wa SADC  ulieleza masikitiko yake makubwa kwa matukio ya vurugu katika nchi za Tanzania na Madagascar zilizosababisha kupotea kwa maisha, pamoja na uharibifu wa mali za umma na miundombinu muhimu.

Katika mkutano huo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwakilishwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ambaye alisema kwamba kwa sasa hali ni shwari nchini Tanzania na kuwa serikali inajipanga kwa mazungumzo kwa ajili ya kuleta mtangamano wa taifa.

Mkutano huo ulikubali uamuzi wa Jamhuri ya Madagascar kuachia wajibu wake kama Mwenyekiti wa SADC kufuatia maendeleo ya kisiasa yaliyoathiri uwezo wake wa kutekeleza majukumu ya nafasi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Jamhuri ya Afrika Kusini ambayo ni naibu katika uongozi SADC kwa sasa imechukua nafasi ya uenyekiti hadi Agosti 2026 kwa mujibu wa katiba ya jumuiya hiyo.

Mkutano huo pia ulikubaliana kuendelea kutekelezwa kwa Kaulimbiu iliyopitishwa katika Mkutano wa 45 wa SADC uliofanyika Antananarivo, Madagascar, mwezi Agosti 2025 isemayo  "Kuendeleza Ukuaji wa Viwanda, Mabadiliko ya Kilimo, na Mpito wa Nishati kwa SADC Imara" hadi Agosti 2026.

Mkutano Maalumu huu wa SADC ulifanyika kwa mwaliko wa Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Matamela Cyril Ramaphosa.

Chapisha Maoni

0 Maoni