Mama Everina Mosses Mmari, mfanyabiashara, ametoa
ushuhuda wa kuhuzunisha kuhusu hasara aliyoipata baada ya duka lake kuchomwa
moto na kutoa wito mzito kwa jamii kuthamini amani na kufanya tathmini ya malezi
ya vijana.
Akisimulia tukio hilo la kutisha, Mama Everina
alisema vijana walivamia duka lake, kumwaga petroli, na kisha kutupa tairi la
moto ndani, na hivyo kusababisha duka lote kuteketea.
"Kwa
kweli sikufanikiwa kuokoa kitu chochote," alisema Mama Everina kwa
masikitiko, akiongeza kuwa alikuwa wakala wa mabenki mbalimbali na kampuni za
simu , simu na mashine za mabenki zimeteketea.
"Simu zote zimeungulia ndani na mtaji wangu
wote umeungulia huko." Hasara hiyo ilihusu pia maduka mawili (fremu ya
kwanza na ya pili) aliyokuwa ameyajaza mizigo.
Mama huyo alisisitiza kuwa vitendo hivyo
haviwakilishi maandamano ya amani bali ni fujo na uhalifu.
"Yale hayakuwa maandamano ni vijana tu
wametokea huko na fujo zao. Kama ni maandamano naamini maandamano huwa hayana
fujo, maandamano ni ya amani."
Mama Everina alimaliza kwa kutoa wito wa dhati kwa
jamii kujikita katika kulea na kushauri vijana, akisisitiza athari za matukio
kama hayo kwa familia:
"Tujaribu kukaa na watoto wetu tuwashauri
maisha yanaendaje kwa sababu leo ni kwangu na watoto wangu, lakini kesho ni kwa
mwingine na watoto wake. Kwa kweli hili jambo linaumiza sana. Tunaomba serikali
mtusaidie kuliangalia hili kwa ukaribu."

0 Maoni