Wananchi wa Kijiji cha Shigela, Wilaya ya Busega
mkoani Simiyu wametakiwa kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari dhidi ya fisi
wanaoripotiwa kuvamia makazi ya watu na kuleta hofu katika jamii.
Rai hiyo imetolewa
Oktoba 6, 2025 na Afisa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (TAWA), Lusato Masinde, wakati wa mkutano wa hadhara
uliofanyika kijijini hapo ambapo timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili
na Utalii, TAWA na Maafisa Wanyamapori wa Halmashauri inaendelea kutoa elimu ya
uhifadhi mkoani humo ili kupunguza madhara yatokanayo na wanyamapori wakali na
waharibifu.
“Tuchukue
tahadhari kubwa, hatuko salama kwa sababu katika mazingira yetu hawa
wanyamapori wapo na kuna vichaka na mapango mengi,” amesisitiza Masinde.
Ameongeza kuwa watoto ndio waathirika wakubwa wa
mashambulizi ya fisi, hivyo wananchi wanapaswa kuwa makini na kuhakikisha
wanawalinda ipasavyo, hasa wakati wa jioni na usiku.
Kwa upande wake, Afisa Maliasili wa Wilaya ya
Busega, Jesca Mathias, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuwasaidia
wananchi wanaokumbwa na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu, ikiwemo
kulipa kifuta jasho na machozi kwa waathirika wa matukio hayo.
“Wananchi wanapaswa kutoa taarifa mapema kuhusu
majeruhi, vifo au uharibifu wa mali unaotokana na wanyamapori. Fomu maalum za
malipo zitajazwa na kupelekwa Wizara ya Maliasili na Utalii ili hatua za kifuta
jasho zichukuliwe kwa wakati,” amesema Jesca.
Naye, Afisa Wanyamapori Mkuu wa Wizara ya Maliasili
na Utalii, Nassoro Wawa, amebainisha kuwa Serikali imeanzisha mfumo wa
kielektroniki wa kukusanya taarifa za wananchi wanaopata athari kutokana na
mashambulizi au uharibifu wa wanyamapori wakali na waharibifu.
“Mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa
wakati. Taarifa zitatumwa moja kwa moja kutoka uwandani kupitia maafisa
wanyamapori, kilimo na mifugo, jambo litakaloharakisha mchakato wa malipo,”
amesema Wawa.




0 Maoni