Wakati
taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025,
mjadala mkali umeibuka miongoni mwa vijana kuhusu umuhimu wa kushiriki
kikamilifu katika upigaji kura. Mfumo wa kidemokrasia unasisitiza kuwa Kura
yako ni haki yako ya msingi, na usipopiga kura utachaguliwa viongozi, lakini
bado kuna kundi kubwa la vijana linaelekea kukaa kimya.
Hoja
iliyoibuliwa hivi karibuni na mmoja wa vijana, Said Nassoro ambaye ana makazi
yake Kawe.
"Kama
nilienda kusimama foleni kujiandikisha daftari la kudumu, kwanini Oktoba 29
nisiende kupiga kura?" Swali hili linafungua mjadala kuhusu utofauti kati
ya kujiandikisha na kupiga kura na kwanini vijana wanahitaji kukamilisha hatua
ya mwisho.
Sababu za Vijana Kukaa Kimya
Licha ya
uhamasishaji mkubwa kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na wadau
wengine kuna wimbi mtandaoni lin
alohimiza vijana kutoshiriki uchaguzi wakimezeshwa taarifa za uongo kuhusu
michakato ya uchaguzi.
Wachambuzi
wa mitandaoni wanasema japo idadi ni ndogo lakini vijana wanaweza kirahisi
kupotoshwa na taarifa za uongo kuhusu michakato ya uchaguzi, jambo linaloweza
kuwafanya waamini kuwa upigaji kura hauna maana.
Nassoro
anasisitiza kuwa kujiandikisha ni ishara ya kwanza ya utayari wa kiraia, lakini
kukamilisha zoezi kwa kupiga kura ndio uamuzi mkuu unaohitajika.
"Kama
ulikuwa na nia njema ya kuchagua kiongozi, kwanini ufanye safari ya nusu kwa
kujitokeza kwenye Daftari, halafu ukatae kukamilisha kwa kutumia kura yako?
Kura yangu ina maamuzi. Inasaidia kwenye mjadala mtandaoni. Badala ya
kulalamika baada ya uchaguzi, ni bora kutumia sekunde chache kwenye sanduku la
kura."
Kina anaungwa
mkono na Joshua Atanazi, kijana mwingine, ambaye alisema: "Kundi la vijana
lina idadi kubwa nchini na ndiyo lenye nafasi ya kufanya mabadiliko chanya
kupitia kura zao. Usipopiga kura, kesho usilalamike."
INEC Yasimama Kidete
Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaendelea kuhimiza vijana na wananchi kwa ujumla
kujitokeza kwa wingi. Kaulimbiu yao inabaki: "UCHAGUZI MKUU OKTOBA 29,
2025. Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura."
Kwa
mujibu wa Tume, upigaji kura ni hatua muhimu ya kutimiza wajibu wa kiraia na
ndio msingi wa kuwa na haki ya kuwawajibisha viongozi baada ya uchaguzi.
Taasisi za dini nchini pia zimehimiza waumini kuombea taifa na kushiriki katika
zoezi hilo la kidemokrasia kwa amani.
Uchaguzi
huu unawaweka vijana katika njia panda: ama waache sauti yao ipotee kwa kukaa
kimya, au waitumie kura yao kama kifaa cha kuamua nani anastahili kuongoza
taifa kwa miaka mitano ijayo. Jibu la swali la Nassoro, kwa mujibu wa INEC na
wadau, ni wazi: Usiache kura yako iishe kwenye foleni ya kujiandikisha.

0 Maoni