Kundi lingine la tembo takribani 50 limeondolewa na
Makamanda wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kutoka maeneo
yaliyokuwa karibu na makazi ya wananchi sanjari na mashamba ya mwekezaji wa
kiwanda cha sukari cha Kagera Sugar jana Oktoba 05, 2025 kuelekea Burigi -
Chato.
Tembo hao waliswagwa na kuvushwa barabara kuu ya
lami inayotokea wilaya ya Misenyi kupitia wilaya ya Karagwe kuelekea Bukoba
wakielekezwa kwenda Hifadhi ya Taifa Burigi–Chato, zoezi hilo la kuwavusha lami
tembo hao halikuwa rahisi baada ya kuona magari yakipishana katika barabara
hiyo.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali
kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo imezielekeza taasisi zake za
uhifadhi kuhakikisha migongano ya muda mrefu kati ya binadamu na wanyamapori
hatari na waharibifu inapunguzwa au kuondolewa kabisa.
Kwa mujibu wa maelezo ya TANAPA yaliyodadavuliwa na
mratibu wa zoezi hilo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Fredrick Mofulu Mkuu
wa Hifadhi ya Taifa Ibanda - Kyerwa alisema kuwa lengo kuu ni kulinda usalama
wa wananchi, mali zao pamoja na kuimarisha uhifadhi endelevu wa wanyamapori,
huku ikiimarisha ushirikiano kati ya jamii na mamlaka za hifadhi.
Aidha, zoezi hilo la kuwaswaga tembo hao takribani
50 kuelekea Burigi - Chato linaendelea leo Oktoba 06, 2025 sambamba na
kusakanya makundi mengine yaliyosalia ili kuhakikisha hakuna tembo wanaobaki katika
maeneo hayo ya wananchi.
Na. Jacob Kasiri - Misenyi
0 Maoni