Katikati
ya mijadala ya kisiasa inayoendelea kuelekea uchaguzi, hatua ya Serikali ya
kuwaita baadhi ya maafisa wa Jeshi la Polisi walio staafu kurejea kazini kwa
mkataba imejikuta ikivutwa kwenye dimbwi la siasa na kupotosha. Hata hivyo,
wachambuzi wa masuala ya usalama wanasisitiza kuwa utaratibu huu si jambo geni
na unalenga kujaza ombwe la utaalamu na uzoefu unaohitajika katika kipindi hiki
nyeti.
Kiapo cha Utii Kinabaki Hai
Kwa
mujibu wa wataalamu wa menejimenti ya vikosi vya usalama, madai kwamba
kurejeshwa kazini kwa wastaafu kunaashiria njama au udhaifu wa kiusalama hayana
msingi wa kiutawala wala kisheria. Kimsingi, askari wa Tanzania huchukua kiapo
cha utii na uaminifu kwa Taifa ambacho, kisheria, kinabaki hai hata baada ya
kustaafu.
Kiapo
hiki huruhusu askari hao kuitwa tena kazini kulingana na mahitaji maalum ya
kitaifa ili kutoa nguvu kazi au uzoefu wa ziada. Hatua hii huonekana katika
nchi nyingi duniani, hasa katika taasisi zinazohitaji utaalamu usiopatikana kwa
urahisi, kama vile jeshi na polisi.
Uzoefu Muhimu Katika Ulinzi wa Uchaguzi
Taarifa
za ndani ya Jeshi la Polisi zinaeleza kuwa kuitwa kwa askari hawa wastaafu,
ambao wengi wao wana uzoefu mkubwa katika kulinda usalama na amani wakati wa
chaguzi zilizopita, ni utaratibu wa kujenga uwezo wa kiutendaji.
Jukumu
kuu la Jeshi la Polisi wakati wa uchaguzi ni kulinda raia na mali zao, kulinda
masanduku ya kura, na kuhakikisha amani inakuwepo. Kwa hiyo, kiongezeko
chochote cha nguvu kazi ya ulinzi, hasa kutoka kwa watu wenye uzoefu wa muda
mrefu, kinalenga kuimarisha amani hiyo na utulivu wa mchakato, na si kuuvuruga.
Kudhibiti Siasa za Upotoshaji
Jaribio
la kutafsiri utaratibu huu wa kawaida wa kiutawala kuajiri wataalamu wastaafu kwa
mkataba kutokana na uhitaji kama propaganda ya chuki au hofu ni hatua ya
kisiasa inayolenga kutafuta kasoro hata katika hatua za msingi za ulinzi wa
Taifa.
Ukweli wa
amani na utulivu wa Watanzania haubadiliki kwa sababu ya taarifa za kupotosha.
Tanzania ina mfumo wa ulinzi unaoheshimu sheria. Kufanya siasa kwa kutumia
mbinu za kuchochea hofu kuhusu usalama wa uchaguzi kunakumbana na ukweli wa
utaratibu uliowekwa kisheria wa Serikali wa kutumia uzoefu wa watumishi wake wa
zamani. Watanzania wengi wanajua thamani ya amani na
hawatadanganywa kwa urahisi.
0 Maoni