Kikosi Cha Nane cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (TANBAT 08), kinacholinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kimetunukiwa Nishani za Ulinzi wa Amani na Umoja wa Mataifa (UN) kutokana na mchango wake mkubwa katika operesheni ya kulinda amani nchini humo chini ya mwavuli wa MINUSCA.
Katika sherehe ya gwaride la heshima iliyofanyika
tarehe 06 Oktoba 2025 mjini Berberati, wanajeshi zaidi ya 500 wa TANBAT 08
wametunukiwa nishani hizo ikiwa ni ishara ya kutambua michango yao katika kuwalinda raia, kusaidia shughuli za
kibinadamu, na kuimarisha utulivu katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.
Uvishwaji wa nishani hizo uliongozwa na Naibu Mkuu wa Vikosi vya Kulinda Amani vya
Umoja wa Mataifa nchini CAR, Meja
Jenerali Maychel Asmi, ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Katika hotuba yake, Meja Jenerali Asmi ametoa
pongezi kwa uongozi, nidhamu na mshikamano mkubwa uliodhihirishwa na TANBAT 08
wakati wa operesheni zao.
“Wanajeshi wa JWTZ wametoa mchango mkubwa sio tu
katika kulinda amani, bali katika kujenga uhusiano mzuri na jamii kwa ujumla.
Huu ni mfano wa kuigwa na vikosi vingine,” alisema Meja Jenerali Asmi.
Naye Kamanda wa TANBAT 08, Luteni Kanali Theofil
Nguruwe, amesema kuwa kutunukiwa nishani hizo ni ushahidi wa uaminifu, juhudi
na uzalendo wa wanajeshi wake katika kutimiza majukumu ya kimataifa.
“Tumehudumu
kwa weledi, heshima na moyo wa kizalendo. Hii ni heshima kwa JWTZ na kwa taifa
letu la Tanzania,” alisema Luteni Kanali Nguruwe.
Sherehe hiyo
imepambwa na maonesho kabambe ya kareti kutoka kikundi maalum cha
makomando wa JWTZ pamoja na burudani ya
ngoma za utamaduni wa Kitanzania kutoka kikundi cha sanaa cha JWTZ, ngoma
zilizowakilisha utambulisho na mshikamano wa taifa la Tanzania jambo lililopokelewa kwa shangwe na wageni
mbalimbali.
Sherehe hiyo pia imehudhuriwa na Maafisa Waandamizi
wa MINUSCA, Maafisa Wanadhimu kutoka Makao Makuu ya JWTZ, viongozi wa Serikali ya CAR, Mashirika ya
Misaada ya Kibinadamu pamoja na wananchi wa Berberati ambao waliwapongeza wanajeshi wa Tanzania kwa
kazi yao ya kujitoa kwa ajili ya amani ya nchi yao.
Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa mataifa
yanayoongoza kwa kutoa vikosi bora vya ulinzi wa amani na kufanya vizuri kwa
zaidi ya miaka 30 ya kushiriki katika operesheni mbalimbali duniani.
0 Maoni