WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa
Serikali imedhamiria kuendelea kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo ili
kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula katika
ukanda wa Afrika Mashariki.
Amesema
lengo la Serikali ni kuendelea kuimarisha usalama wa chakula, kupunguza
utapiamlo na kuijenga Tanzania yenye wananchi wenye afya bora, nguvu kazi imara
na uchumi unaojitegemea.
Amesema
hayo leo Alhamisi (Oktoba 16, 2025) wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya
Chakula Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Mkoani Tanga, kwenye uwanja wa Shule
ya Sekondari Usagara.
“Pamoja
na mipango hiyo, Serikali itaendelea kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji,
ushirikiano, na ubunifu, ili kuhakikisha nchi inakuwa na chakula cha kutosha
kwa matumizi ya ndani na ziada kwa mauzo ya nje.”
Amesema
kuwa Serikali katika kuhakikisha imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya
kilimo, iliongeza bajeti ya sekta hiyo kutoka shilingi bilioni 246 mwaka
2020/2021 hadi kufikia shilingitrilioni 1.3 mwaka 2024/2025.
“Matokeo
ya jitihada hizini dhahiri: uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka
tani milioni 18 mwaka 2020/2021 hadi tani milioni 22 mwaka 2023/2024, huku
kiwango cha utoshelevu wa chakula kikiongezeka kutoka asilimia 114 hadi 128
mwaka 2024/2025”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi
vijana nchini wajikite zaidi katika kilimo, ufugaji na uvuvi wa kisasa Kwa kuwa
sekta ya kilimo ni tegemeo kubwa la ajira. “Serikali imeweka mazingira mazuri
ya mikopo, ruzuku, na huduma za ugani ili vijana wawe sehemu ya mapinduzi ya
kilimo chenye tija”.
Pia,
Mheshimiwa Majaliwa amewahimiza wakulima, wafugaji na wavuvi kuhakikisha kuwa
baada ya mavuno, waongeze thamani ya mazao kupitia usindikaji na ubunifu,
badala ya kuuza mazao ghafi. “Ukiongeza thamani kipato kinakuwa kikubwa zaidi
na kinaimarisha usalama wa chakula, na kupunguza upotevu wa mazao unaosababisha
hasara kwa wazalishaji.”
Mheshimiwa
Majaliwa pia alizipongeza sekta binafsi pamoja na Mashirika ya Kimataifa kwa
kuwezesha wakulima wengi kufikiwa na teknolojia za kisasa, mikopo nafuu, na
huduma za ugani zilizo bora zaidi. “Ninawashukuru pia wadau wa sekta binafsi,
wakiwemo wazalishaji wa pembejeo, viwanda vya usindikaji, taasisi za fedha, na
wajasiriamali wadogo, ambao wanashiriki kikamilifu katika kuongeza uzalishaji
na kuhakikisha mazao yanapata masoko yenye uhakika”.
kwa Upande
wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweri amesema kuwa kazi kubwa
imefanywa na Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan katika uwekezaji kwenye sekta ya kilimo iliyowezesha kuifanya nchi kuwa
na usalama wa kutosha wa Chakula.
Naye
Muwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania Suzan Namondo ameipongeza
Tanzania kwa hatua kubwa iliyoipiga katika masuala ya kilimo pamoja na usalama
wa chakula.
“Kupitia
uongozi bora na uwekezaji Tanzania imeongeza kiwango cha uzalishaji wa chakula
na kuwezesha nchi hiyo kupiga hatua kubwa katika utoshelevu wa chakula, hii
inaonesha namna Tanzania iliyo mchangiaji mkubwa katika usalama wa chakula
Afrika Mashariki”
Ameongeza
kuwa chakula si suala la uzalishaji pekee, bali linahusu watu na mfumo mzima wa
chakula unaounganisha kile tunacholima, namna tunavyokichakata, na iwapo mfumo
huo ni mzuri kwa ustawi binadamu pamoja
na kulinda mazingira yetu.
Kaulimbiu
ya maadhimisho hayo ni “Tuungane Pamoja Kupata Chakula Bora Kwa Maisha Bora Ya
Baadaye.” ambayo inasisitiza kuwa masuala ya lishe bora, utunzaji wa chakula,
na matumizi sahihi ya mazao ya chakula ni jukumu la kila mmoja.


0 Maoni