Wananchi kutoka mikoa mbalimbali wameonyesha nia thabiti ya kushiriki katika uchaguzi nkuu 2025 na kulinda amani ya taifa. Kauli zao zinasisitiza kwamba uchaguzi si vita, bali ni zoezi la kikatiba linalopaswa kutekelezwa kwa utulivu.
Bwana Emmanuel Petro, dereva wa Bodaboda kutoka Amani Tumbo, Bagamoyo, alifanya ujumbe kuwa rahisi: "Kura yako ni silaha ya amani. Oktoba 29, 2025, ni siku ya kura, amani, na umoja wa Taifa."
Daudi Bartazar Moyo, mkazi wa Udindivu, Bagamoyo, alithibitisha: "Ni vyema kwenda kupiga kura na mimi nitaenda. Kisha nitarejea nyumbani kuendelea na majukumu yangu ya kila siku." Kauli hii inamaanisha maisha ya kawaida hayapaswi kukatizwa na uchaguzi.
Mwanaidi Stefano Stanley wa Kibaha kwa Mathiasi, alionyesha imani yake: "Nitaamka asubuhi na mapema kwenda kupiga kura. Nawasihi Watanzania kujitokeza kwa wingi. Ninaamini uchaguzi utakuwa wa amani, haki, na huru."
Emiliana Damson wa Kibaha naye anatarajia kutumia haki yake kumchagua kiongozi anayemtaka yeye na familia yake, huku akitarajia utulivu utaendelea kutawala.
Kura Ni Wajibu, Utulivu Ni Lazima
Wito wa kurejea nyumbani mara baada ya kupiga kura una lengo la wazi: kuiacha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ifanye kazi yake kwa uhuru na usalama. Kufuata utaratibu huu kumlinda kila mpiga kura na kuzuia mikusanyiko isiyo ya lazima ambayo inaweza kutumiwa na wachochezi kuvuruga amani.
Kama alivyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: "Kura ni silaha ya msingi ya kila Mtanzania kuamua mustakabali wa Taifa lake."
Oktoba 29, tuoneshe ukomavu wetu: Toka, Tiki, na Rudi Nyumbani. Linda kura yako, linda amani ya nchi yako.

0 Maoni