Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeridhishwa na hali ya usalama iliyopo
nchini huku taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe
28 na 29 Oktoba, 2025. Jeshi limehakikishia Watanzania wote hali ya Amani,
Usalama na Utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, wakati wa
uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Kupitia
taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na
Uhusiano wa JWTZ, Kanali Bernard Masala Mlunga , Jeshi lilitangaza kuwa
linaendelea kufuatilia kwa karibu na kutathmini hali ya Ulinzi na Usalama
nchini.
Msemaji
huyo alisema kwamba JWTZ linaridhishwa na jinsi Vyama vya Siasa vinavyoendesha
kampeni zao kwa kuzingatia matakwa ya kisheria, kuheshimiana na kuvumiliana
kunakooneshwa kupitia kwa wagombea wao wa ngazi za Uraisi, Ubunge na Udiwani.
Jeshi limetoa ombi kwa vyama vya siasa kuendeleza hali ya amani na utulivu
wakati wote wa kampeni, kupiga kura na baada ya kupiga kura.
Aidha,
Jeshi lililipongeza Jeshi la Polisi na Vyombo vingine vya Usalama kwa jinsi
vinavyoendelea kusimamia hali ya usalama katika kipindi hiki. Pia limewapongeza
wananchi kwa kuendelea kutumia haki yao ya msingi ya kushiriki kwa amani na
utulivu katika kusikiliza sera za vyama mbalimbali.
Onyo kwa
Wachochezi
Pamoja na
hali ya amani iliyopo, Kanali Mlunga alisema kuwa kumeendelea kujitokeza baadhi
ya watu wanaojiita wanaharakati kutoka ndani na nje ya nchi kutumia mitandao ya
kijamii kupotosha Umma kwa kuweka maudhui yenye kuleta uchochezi. Wachochezi
hao wanajaribu kulihusisha Jeshi na siasa ili kutimiza azma yao ya uvunjifu wa
amani.
Jeshi
linauomba Umma wa Watanzania kupuuza machapisho au taarifa ambazo zimekua
zikionekana kwenye mitandao ya kijamii. Wananchi wanakumbushwa kuwa taarifa
zote zinazolihusu Jeshi zitatolewa na Makao Makuu ya Jeshi kwa utaratibu rasmi
wa mawasiliano ya Jeshi na Umma.

0 Maoni