MAKAMU wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, amezindua rasmi
Makumbusho ya Urithi wa Kijiolojia ya Ngorongoro–Lengai, yaliyogharimu zaidi ya
Sh. bilioni 35 ambayo yanatarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa utalii wa
kihistoria na kielimu nchini.
Makumbusho
hayo yapo katika eneo la Ngorongoro–Lengai Geopark, linalotambuliwa na Shirika
la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama Geopark pekee
Kusini mwa Jangwa la Sahara na ya pili barani Afrika.
Akizungumza
leo Oktoba 16,2025 katika uzinduzi huo wilayani Karatu, Dkt. Mpango amesema
kukamilika kwa makumbusho hayo ni hatua muhimu katika kukuza utalii wa urithi
na historia, sambamba na kutangaza vivutio vya asili vya Tanzania kimataifa.
“Geopark hii siyo tu hifadhi ya historia, bali
ni chachu ya elimu, tafiti na maendeleo ya jamii zinazozunguka eneo hili,”
amesema Dkt. Mpango.
Dkt.
Mpango ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha shughuli zote za
utalii katika eneo hilo zinafanyika kwa kuzingatia misingi ya uhifadhi na
uendelevu wa mazingira, akisisitiza kuwa uharibifu wa mazingira unaweza
kuathiri moja kwa moja ustawi wa sekta ya utalii.
Pia,
ameagiza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kutoa mafunzo kwa watumishi
watakaohudumu katika Geopark hiyo ili kuongeza ufanisi na ubora wa huduma kwa
wageni.
Kwa
upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema mradi huo
ni wa kwanza wa aina yake barani Afrika chini ya mpango wa “Belt and Road
Initiative”, na unadhihirisha ushirikiano wa kimkakati kati ya China na
Tanzania katika nyanja za utalii na utamaduni.
Naye
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema eneo la
Ngorongoro–Lengai limetambuliwa na UNESCO na pia limepata tuzo ya kivutio bora
cha utalii Afrika kupitia World Travel Awards 2025 ni ishara ya mafanikio ya
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri
Chana ameongeza kuwa mafanikio mengine makubwa ni pamoja na TANAPA na NCAA
kupatiwa kibali cha kutumia hadi asilimia 51 ya mapato yao katika mwaka wa
fedha 2025/26.
Kadhalika,
amesema kuongezeka kwa watalii wa kimataifa kutoka 1,808,205 mwaka 2023 hadi
2,142,895 mwaka 2024, Watalii wa ndani wameongezeka kutoka 1,985,707 mwaka 2023
hadi kufikia 3,217,352 mwaka 2024.




0 Maoni