Katibu
Mkuu wa Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, ametoa wito kwa watendaji wa
Tume ya Madini nchini kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uongezaji thamani ya
madini ili kuongeza ajira, kukuza fursa za kiuchumi na kuimarisha mchango wa
Sekta ya Madini katika Pato la Taifa.
Akizungumza
leo, Oktoba 15, 2025, jijini Tanga katika kikao cha menejimenti ya Tume ya
Madini kilichoshirikisha Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo,
Makamishna wa Tume ya Madini Mhandisi Theonestina Mwasha na Dkt. Theresia
Numbi, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo,
Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Mhandisi Samamba
amesema kuwa Sekta ya Madini ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi endapo
uongezaji thamani utawekewa kipaumbele.
“Mnapoweka
mazingira rafiki ya uwekezaji kama vile kurahisisha upatikanaji wa vibali na
miundombinu, wawekezaji wanaongezeka, ajira zinapatikana, mapato ya Serikali
yanaongezeka na uchumi unakua,” amesema Mhandisi Samamba.
Amesisitiza
Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kushirikiana na viongozi wa mikoa na taasisi
nyingine za Serikali kuhakikisha mazingira ya uwekezaji kwenye viwanda vya
uongezaji thamani wa madini yanakuwa wezeshi, ili kuvutia wawekezaji wa ndani
na nje ya nchi.
Katika
hatua nyingine, Mhandisi Samamba amewataka Maafisa hao kuendelea kuwajengea
uwezo wachimbaji wadogo kwa kuwapatia elimu ya Sekta ya Madini, taarifa za
kijiolojia kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST),
kuwaunganisha na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na taasisi za
kifedha ili kuongeza tija na mapato yao.
“Ninaamini
tukiwasaidia wachimbaji wadogo wataongeza ajira, kukuza mzunguko wa fedha na
kuiwezesha Serikali kukusanya kodi zaidi kwa ajili ya kuboresha huduma za
kijamii kama elimu, afya, barabara na maji,” amesisitiza.
Aidha,
ameitaka Tume ya Madini kuendelea kutoa elimu kwa Chama cha Watoa Huduma kwenye
Migodi (TAMISA) ili kuongeza ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini
kupitia mpango wa Local Content.
Vilevile,
amewataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha usalama kwenye shughuli za
uchimbaji wa madini kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu ili
kuepuka ajali na uharibifu wa mazingira. Pia amesisitiza umuhimu wa kusimamia
haki katika utatuzi wa migogoro ya wachimbaji wadogo.
Mhandisi
Samamba amehitimisha kwa kuwataka watumishi wote wa Tume ya Madini kushiriki
kikamilifu katika zoezi la uchaguzi litakalofanyika Oktoba 29, 2025, nchi
nzima.
Kwa
upande wao, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo na Katibu
Mtendaji, Mhandisi Ramadhani Lwamo, wameishukuru Wizara ya Madini kwa kuendelea
kuiwezesha Tume kupitia vitendea kazi ikiwemo magari, pikipiki, fedha na
rasilimaliwatu, hali iliyochangia ongezeko la makusanyo ya maduhuli mwaka hadi
mwaka.
Wamesema
katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Julai–Septemba), Tume ya
Madini imekusanya Shilingi Bilioni 315.4 sawa na asilimia 105.13 ya lengo la
Shilingi Bilioni 299.99, na kuwataka Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuongeza
ubunifu na juhudi ili kufikia na kuvuka lengo la Shilingi Trilioni 1.2 kwa
mwaka wa fedha 2025/2026.




0 Maoni