Zaidi ya wakandarasi wazawa 276 wameanza kunufaika na mikopo
yenye gharama nafuu, kupitia fedha zilizopatikana kutokana na Hati Fungani ya
Miundombinu (Infrastructure Bond) iliyoanzishwa mwaka 2024.
Mpango huu wa ubunifu wa kifedha ni sehemu ya juhudi zenye
maono za serikali za kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa mitaji miongoni
mwa wakandarasi wa ndani, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu na kwa ufanisi
katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya nchi.
Ni muhimu sana kwa kila Mtanzania kutambua umuhimu wa kupiga
kura kwa uwazi na kwa dhamira ya dhati kwa lengo la kuchagua viongozi katika
ngazi zote wenye maono ya wazi kuhusu namna ya kutumia rasilimali zetu
kuwajenga wazawa na kuimarisha taifa.
Maamuzi yetu ya kisiasa ndiyo yanayoamua kama mipango kama
hii ya Hati Fungani ya Miundombinu itaendelezwa na kuimarishwa, au kuachwa.
Chagua viongozi wanaouthamini na kuuendeleza uzalendo wa kiuchumi.
Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa hadi sasa, Shilingi Bilioni
323.09 zimekusanywa kupitia hati fungani hiyo, ikiwa ni sawa na asilimia 215.4
ya lengo lililowekwa awali la kukusanya Shilingi Bilioni 150. Hii inaonyesha
imani kubwa ya wananchi na taasisi katika mpango huu. Kati ya fedha hizo,
Shilingi Bilioni 223.8 zimeombwa na kugawiwa kwa wakandarasi wazawa 276 nchini kote.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za
Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff, fedha hizi zimeanza kutumika
rasmi katika utekelezaji wa mikataba ya matengenezo na ujenzi wa barabara
katika maeneo mbalimbali nchini.
Hii ni hatua muhimu inayowezesha wakandarasi wetu wazawa
kutekeleza majukumu yao kwa wakati, huku ikipunguza utegemezi wa mitaji kutoka
nje na kuimarisha uchumi wa ndani.
Kupitia Hati Fungani hii ya Miundombinu, wakandarasi wazawa
sasa wanapata fursa ya kupata dhamana za kazi zinazohitajika wakati wa
utekelezaji wa mikataba yao, jambo linalorahisisha utekelezaji wa miradi kwa
ufanisi zaidi.
Miradi ya barabara, ikiwa ni uti wa mgongo wa miundombinu ya
Taifa, inachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa kuboresha huduma za
usafiri na usafirishaji, jambo linalonufaisha moja kwa moja wazawa wote.
Benki ya CRDB inashirikiana na TARURA kuhakikisha kuwa fedha
zilizokusanywa zinatumika kwa ufanisi. Benki hiyo pia inahusika katika utoaji
wa mikopo kwa wakandarasi wazawa, hatua inayowawezesha kukabiliana na
changamoto za kifedha.
Kwa ujumla, mpango huu wa ubunifu wa kifedha umeongeza uwezo
wa wakandarasi wazawa, umeimarisha sekta ya miundombinu ya barabara, na
umeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.
Mafanikio haya yanathibitisha thamani ya maono makubwa na
ubunifu wa kifedha kutoka kwa viongozi wetu. Miradi na mipango ya namna hii,
ambayo inawalenga na kuwaamini wazawa, ndiyo inayobadilisha sura ya uchumi wetu
na kuleta ustawi wa kudumu.

0 Maoni