Mgombea
wa Ubunge Jimbo la Rufiji Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema endapo wananchi
watampa ridhaa ya kumchagua tena katika kipindi atahakikisha kwa pamoja
wanafanya ujenzi wa uchumi kwa kila mwanarufiji wa jimbo hilo ili kuendelea
kuboresha maisha yao.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara wa kukiombea kura Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye
Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu kwa ngazi ya Urais, Ubunge na
Udiwani katika kata ya Muhoro jimboni Rufiji jana Mhe. Mchengerwa amesema katika kuhakikisha
miradi mingi ya maendeleo inakwenda kutekelezeka atakwenda kuiomba serikali kuweka kituo cha kupozea umeme ili kuwa na
umeme wa uhakika ili kusaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kilimo
ambayo tayari wawekezaji wameshajitokeza.
“Tayari
tumepata wawekezaji wanaokwenda kujenga viwanda vikubwa hapa Rufiji, tarafa ya Muhoro, tumeshapata
muwekezaji mkubwa ambaye anakwenda kuwekeza
zaidi ya shilingi trioni 1.3 kwenye
kiwanda kikubwa cha ndizi hali ambayo itatufanya kuuza
ndizi duniani”. Amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Amesema akina mama zaidi ya 1000 na vijana zaidi ya 6000 wanakwena kujipatia
ajira kwenye mradi
huu ambapo amefafanua kuwa viwanda
vitano vinakwenda kujengwa kwenye
tarafa hiyo ya Muhoro na kuleta
ajira nyingi kwa wananchi.
Ametoa wito kwa
vijana na wananchi kujiandaa kimtizamo
na kuwa tayari kufanya kazi kwa bidi
ili wawekezaji hao waweze
kuwaajiri badala ya kutegemea watu kutoka nje ya maeneo hayo.
Aidha
amewashukuru kwa wananchi hao kuendelea kumchagua
katika vipindi vyote kwa kura
nyingi na kufafanua kuwa wamekuwa wakimchagua kwa kuwa wamejenga imani kubwa kuwa ni mtumishi wao ambaye siku zote amekuwa
na ndoto za kuwaletea maendeleo ya
kweli.
Leo, Mhe.
Mchengerwa anaendelea na mikutano ya hadhara katika kata nyingine za Jimbo hilo
kuomba kura kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa madiwani na kwake mwenyewe ili
apewe ridhaa ya kuwaongoza tena katika kipindi hiki.
Mhe.
Mchengerwa ni Mbunge wa tisa wa kuchaguliwa katika jimbo hilo la Rufiji toka
lianzishwe na kuongozwa na wabunge kadhaa kuanzia mwanasiasa mkongwe nchini
hayati Bibi Titi Mohamed ambapo
anaelezewa kuwa ni miongoni mwa wabunge walioliletea maendeleo makubwa Jimbo
hilo ukilinganisha na wabunge waliotangulia.
Miongoni mwa mafanikio makubwa
yaliyoletwa na Mhe. Mchengerwa
katika kipindi chake ni pamoja na ongezeko kubwa la Shule za Msingi na
Sekondari, zahanati, vituo vya afya na Hospitali, ujenzi wa madaraja, barabara,
huduma za maji na kuvutia wawekezaji
katika jimbo hilo.
Na. Yohana Kidaga- Muhoro, Rufiji




0 Maoni