Serikali
kwa Kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), kupitia
ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) watazindua Viwango Fanisi vya Chini vya Nishati
(Minimum Energy Performance Standards – MEPS) na Maabara za Upimaji wa Ufanisi
wa Nishati.
Uzinduzi
huo utafanyika kesho tarehe 16 Oktoba 2025, jijini Dar es Salaam katika Makao
Makuu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Kamishna
na Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amesema hayo leo
wakati akizungumza na Waandishi wa
Habari jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa maabara
hiyo ni kuhakikisha kuwa vifaa
vinavyotumika nchini vinatumia nishati kwa ufanisi kwa lengo la kupunguza
gharama kwa watumiaji na kulinda mazingira dhidi ya uzalishaji wa hewa ukaa.
Ameongeza
kuwa juhudi hizo zitasaidia kupatikana kwa umeme wa ziada kwenye gridi ya taifa
na kutumika katika maeneo mengine ya nchi yenye upungufu wa umeme na kuweza
kuwafikia wateja wengine wapya.
Amesema
kupitia mradi huo, Tanzania itazindua viwango vya kwanza vya chini vya matumizi
ya nishati ya umeme vinavojulikana kama MEPS kwa vifaa vitano vya kipaumbele
ambavyo vinachangia matumizi makubwa ya umeme ambavyo ni Viyoyozi Majokofu,
Runinga, Feni pamoja na Mota za umeme.
“Watu
wengi wamekuwa wakitumia vifaa mbalimbali majumbani na maeneo mengine bila
kufahamu kiwango halisi cha umeme kinachotumika katika vifaa, hivyo kuwepo kwa
maabara hiyo nchini, kutasaidia kupima vifaa hivyo na kujua matumizi fanisi ya
nishati na hivyo kuokoa gharama katika matumizi,” amesema Mha. Luoga
Mha.
Luoga amesema kuwa maabara hizo zitakuwa na jukumu la kupima na kuthibitisha
ubora na ufanisi wa vifaa vya umeme vinavyoingizwa nchini, kudhibiti bidhaa
duni zisizo na viwango,kutoa ithibati kwa wazalishaji wa ndani na kusaidia
Serikali katika usimamizi wa soko.
Mha.
Luoga amefafanua kuwa maabara hizo zinathamani ya zaidi ya Euro milioni 1.8
(takriban shilingi bilioni 5).
Amesema
kwa mara ya kwanza, Tanzania itakuwa na uwezo wa ndani wa kuhakikisha bidhaa
zote zinakidhi viwango vya kitaifa na vya kikanda kabla ya kufika kwa mlaji.
Amesema
uundaji wa viwango hivyo umehusisha Wataalam kutoka taasisi zaidi ya 10
zikiwemo Wizara ya Nishati, TBS, TANESCO, EWURA, REA, TIRDO, DIT, UDSM, ATC,
NCC, TAREA na sekta binafsi.
Ameongeza
kuwa kwa ushirikiano wa kitaalamu na Mshauri wa Kimataifa, viwango vya kiyoyozi
na majokofu vimeidhinishwa rasmi kuwa viwango vya Kikanda vya Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC), hatua inayowezesha Tanzania kuwa sehemu ya soko la kikanda
lenye bidhaa zenye ubora na ufanisi wa nishati.
Uanzishaji
wa MEPS na maabara hizi unalenga kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Nishati ya
Taifa (2015), Mkakati wa Taifa wa Matumizi Bora ya Nishati (NEES 2024–2034) na
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Katika
hatua nyingine , Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeanza juhudi za
kuandaa viwango katika teknolojia ya kupikia kwa kutumia nishati Safi ili kuendana na Mkakati wa Taifa wa
Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034).
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Metrolojia wa TBS, Ridhiwani
Matange ametoa wito kwa watanzania kutumia vifaa ambavyo vitakuwa vimepimwa
katika maabara hizo.
Amesema
elimu zaidi itatolewa kwa wananchi ili kuwajengea uwezo wa uelewa juu ya
maabara hizo na viwango fanisi vinavyohitajika katika matumizi yao ya kila
siku.
Naye Mkuu
wa Ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, Arc Stalmans na Msaidizi wa Mwakilishi Mkazi,
Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP) Gertrude Lyatuu waamesisitiza kuwa wataendela kushirikina na Serikali ya
Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hususan mradi huo wa
matumizi bora ya nishati ili kupunguza hewa ya ukaa ili kulinda Mazingira.



0 Maoni