Mgombea Udiwani CCM kata ya Nyandira aahidi ushirikishaji wananchi kuleta maendeleo

 

Mgombea Udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nyandira, Ndugu Magari Nesto, ameendeleza kunadi Ilani ya chama chake huku akisisitiza ushirikishaji wa wananchi na serikali katika kupaisha maendeleo ya kata ya  Nyandira.

Alitoa kauli hiyo katika kampeni zake zinazoendelea katika kata hiyo wakati alipofanya mkutano wenye mafanikio makubwa katika Kijiji cha Nyandira hapo jana, Oktoba 4, 2025.

Mkutano huo, ambao mgombea huyo ameuelezea kuwa "mkutano bora kwa tarafa ya Mgeta na Mlali tangu kuanza kwa kampeni," ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakuu wa chama, akiwemo Mbunge mtarajiwa wa Wilaya ya Mvomero, Bi. Sara Msafiri Ally, pamoja na viongozi wa kamati ya siasa ya Wilaya ya Mvomero, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Mkoa, na Mjumbe mmoja kutoka Taifa.

Katika mikutano yake yote aliyofanya tangu kuzindua kampeni, Ndugu Magari Nesto amesisitiza ushirikishwaji wa wananchi na serikali katika kutatua matatizo yanayokabili kata hiyo. Kampeni zake zimejikita katika kutembelea na kukutana na wananchi katika vijiji vya Mwarazi (ambapo alizindua kampeni), Kibuko, na sasa Nyandira.

Katika hotuba zake, mgombea huyo ametaja vipaumbele kadhaa vya kimaendeleo,ikiwamo elimu, miundombinu, uchumi,masoko, utalii na mazingira.

Elimu: Kuboresha utoaji elimu wenye ubora na kuimarisha mazingira bora ya shule za msingi na sekondari.

Miundombinu: Kushughulikia changamoto za mawasiliano, hasa katika uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Uchumi na Masoko: Kufanya juhudi za kuimarisha masoko ya bidhaa za wananchi wa Nyandira.

Utalii na Mazingira: Kuendeleza uwezekano wa kuendesha utalii na kuhifadhi misitu kwa ajili ya kurejesha hali ya hewa ya zamani.

Akizungumzia mafanikio ya mikutano hiyo, hasa ule wa Nyandira, Ndugu Magari Nesto aliwashukuru kwa dhati wananchi na viongozi wa Kata ya CCM kwa kujitoa kwao.

"Hakika haikuwa rahisi kabisa kwasababu ya taratibu za Chama Chetu kwa jukumu la aina hii kuandaliwa na Uongozi wa CCM kata, ambapo kwa 100% ninyi ndugu zangu kwa michango yenu ndio imesaidia sana kufanyika vyema jambo hili kwa kiwango hiki," alisema.

Alisema kuwa rekodi ya mkutano huo na mingine ina maana kubwa sana kwao na kwa heshima ya kata yao, akitarajia kupata ridhaa ya wananchi ili waanze kuwatumikia.

Mgombea Udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Nyandira,tarafa ya Mgeta mkoani Morogoro, Ndugu Magari Nesto , akiomba kura kwa staili ya aina yake wakati wa kampeni za kuomba ridhaa za wananchi kuwa diwani wa kata hiyo Oktoba 4, mwaka huu. (na Mpiga picha wetu).



Chapisha Maoni

0 Maoni