Kamishna
wa Uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro Bw Abdul-Razak Badru amefungua mafunzo kwa
wadau wa uwekezaji katika sekta ya utalii kuhusu mfumo mpya wa kidijitali wa Makazi Online
Portal (MoPO) kwa lengo la kuongeza uwazi na usawa katika upangaji wa makambi
ya kulala wageni (Campsites) hususan eneo la Ndutu Ngorongoro.
Akifungua
mafunzo hayo Kamishna Badru ameeleza kuwa hatua ya kubuni mfumo mpya wa Makazi
Online Portal inalenga kuboresha huduma kwa wateja katika sekta ya uhifadhi na
utalii kwa kujikita kwenye matumizi ya
teknolojia kwa huduma ambazo wadau hao wanazihitaji katika eneo la
hifadhi ya Ngorongoro.
“Mfumo tulioubuni kwa dunia ya sasa ni muhimu
katika kuboresha huduma kwa misingi ya
uwazi, haki na ufanisi, tunaamini kila mdau atapata huduma nzuri na kwa
wakati bila upendeleo,” alisema Kamishna Badru.
Wakati wa
mafunzo hayo Wataalam wa TEHAMA na Uwekezaji walitoa semina kwa washiriki
kuhusu matumizi ya mfumo wa Makazi Online Portal ikihusisha namna ya kuomba nafasi za makambi, kufuatilia
maombi, na kupata taarifa ya maombi yao kwa wakati.
Mfumo wa
Makazi Online Portal uliohudhuriwa na wadau wa uwekezaji katika sekta ya
utalii zaidi ya 150 unatarajiwa kuwa
suluhisho la muda mrefu katika kuomba kuwekeza makambi ya kulala wageni eneo la
Ndutu tofauti na mfumo wa zamani wa
kutuma barua ya maombi kwa kamishna wa Uhifadhi hali inayoongeza uwazi wa kufuatilia
maombi na ufanisi katika upangaji wa kambi hizo.



0 Maoni