Na. Veronica Simba - WMA
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Bw. Alban Kihulla amewaambia Waheshimiwa Wabunge kuwa WMA hufanya uhakiki wa mitungi ya gesi ya kupikia inayouzwa nchini ili kujiridhisha kuhusu ujazo wake kabla ya kuingia sokoni.
Akizungumza katika semina kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuhusu majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara na Taasisi zake iliyofanyika Mei 13, 2026 Bungeni Dodoma, Kihulla alisisitiza kuwa jukumu la WMA ni kuhakiki na kusimamia usahihi wa vipimo katika sekta zote, ikiwemo nishati.
Hata hivyo
amewahimiza wananchi wakiwemo wabunge kuchukua tahadhari zaidi wakati
wa kununua gesi.
“Kabla ya kununua gesi, hakikisheni mtungi
huo unapimwa na muuzaji mbele yenu ili kujiridhisha kuhusu ujazo
wake. Epukeni kununua gesi kutoka kwa wauzaji wasio na mizani, kwa
sababu hutaweza kujua kama gesi uliyonunua ina ujazo sahihi kama
ilivyoandikwa kwenye mtungi”, alisema Kihulla.
Akitoa
mwongozo wa jinsi ya kutofautisha uzito ulioandikwa kwenye mtungi,
Kihulla ameeleza kuwa kila mtungi wa gesi una maelezo mawili muhimu
ya uzito ambayo mwananchi anapaswa kuyafahamu ambayo ni Net Weight na
Gross Weight.
“Net Weight ni uzito wa gesi pekee iliyomo
ndani ya mtungi. Hii ndiyo kiasi unacholipa. Gross Weight ni uzito wa
gesi pamoja na uzito wa mtungi tupu.”
Alisema wakati muuzaji
anapima mtungi uliojaa gesi, mnunuzi anapaswa kuangalia kama uzito
unaooneshwa kwenye mzani unalingana na jumla ya net weight
iliyoandikwa kwenye mtungi pamoja na uzito wa mtungi tupu. Ikiwa
mzani unaonesha chini ya jumla hiyo, basi kuna upungufu wa
gesi.
Amesema changamoto iliyopo kwa sasa ni kuwa wananchi
wengi bado hununua gesi kwa mazoea bila kujali kama muuzaji ana mzani
na amepima mtungi huo au la.
Pia amebainisha kuwa baadhi ya
wananchi huagiza vijana wa bodaboda kuwanunulia gesi ili kurahisisha
usafirishaji, bila wao wenyewe kuwepo ili kujiridhisha. Hali hiyo
inawafanya kukosa uhakika kuhusu ujazo halisi wa gesi
wanayonunua.
Katika ufafanuzi wake, Kihulla pia amezungumzia
upimaji wa tochi za barabarani zinazotumiwa na askari kupima mwendo
wa magari. Amesema WMA huhakiki tochi hizo ili kuhakikisha zinapima
kwa usahihi na haki inatendeka kwa wamiliki wa magari.
“Hata
hivyo, nawasihi wananchi kuwa endapo mtatilia shaka au kubaini kuna
tatizo la usahihi wa vipimo popote pale, msisite kuwasiliana na WMA
kwa hatua za haraka,” alisema.
Awali, kupitia wasilisho la
video, Kihulla alieleza kuwa WMA inasimamia matumizi sahihi ya vipimo
katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, miundombinu, madini,
maji, ujenzi, nishati na usafiri.
Aidha, alisema Wakala hiyo
inajiandaa kuanza uhakiki wa vipimo katika maeneo mapya ikiwemo sekta
ya mawasiliano hususan kuhakiki usahihi wa bando za intaneti na
dakika za simu zinazotolewa na makampuni ya mawasiliano ili kuongeza
wigo wa ulinzi wa mwananchi.
Amesema, lengo ni kuhakikisha
mteja anapata kiasi halisi cha data au dakika alichonunua, bila
kupunguzwa au kupotea kabla ya muda wake kuisha.



0 Maoni