WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amekutana na Rais wa Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Patrick Herminie mara
baada ya kuapishwa na akatumia nafasi hiyo kuwasilisha salamu za pongezi kutoka
kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Waziri Mkuu Majaliwa
amesema leo (Jumatatu, Oktoba 27, 2025) kwamba katika mambo ya msingi ambayo
Rais Dkt. Samia alitaka yawasilishwe ni uhakika wa Tanzania kuendelea kuiunga
mkono Jamhuri ya Shelisheli na kuwapongeza wananchi wake kwa uamuzi walioufanya
kupitia uchaguzi wao wa kidemokrasia na kuwawezesha kumpata Rais mpya.
“Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia alitaka pia nimhakikishie Rais Dkt. Herminie kwamba Tanzania itaendelea
kufanya kazi na Shelisheili ikiwa ni kuunga mkono jitihada za waasisi wa
mataifa haya kuendeleza ushirikiano kwenye nyanja za uchumi, ulinzi, siasa,
biashara na uwekezaji.”
Amesema Rais wa
Shelisheli ameridhia kuanzishwa kwa Tume ya Ushirikiano ya Pamoja (JPC)
itakayotoa fursa kwa watalaamu wa nchi hizo mbili kukutana na kuratibu kwa
pamoja masuala kutoka kwenye sekta na wajadili kwa kina mahitaji ya mahusiano
kutoka nchi hizi mbili. “Tuna mahusiano katika wizara za elimu, afya, ulinzi na
kibiashata hasa usafirishaji wa anga na utalii.
Amesema kauli ya Rais
mpya wa Shelisheli imeleta matumaini kwamba Tanzania sasa imepata rafiki ambaye
atahuisha mahusiano ambayo yalikuwepo hapo awali. “Rais huyu ameleta mwelekeo
mpya alipozungumzia kuwa chama chake kilikuwa na urafiki wa muda mrefu na Chama
cha Mapinduzi. Hivyo tunaamini chama chake cha United Seychelles (US)
kitaimarisha mahusiano na Chama cha Mapinduzi na kufanya vyama vyetu kuwa
imara.”
Waziri Mkuu amesema
kuwa Rais Dkt. Herminie ambaye aliapishwa jana kuwa Rais wa sita wa nchi hiyo,
alishawahi kuwa Spika wa Bunge la Seychelles na alishafanya ziara kadhaa nchini
miaka ya nyuma. Hivyo anaielewa Tanzania kwa ubora na umahiri wake katika
masuala mbalimbali.
Mapema, Waziri Mkuu
alikutana sekretarieti ya wanadiaspora wa Shelisheli ambao walimweleza fursa
zaidi za uwekezaji zilizomo nchini humo hasa katika maeneo ya utalii, ajira
kwenye sekta za afya, elimu, kilimo cha bustani na waongoza utalii.
Amewataka wazingatie
taratibu na sheria za nchi waliyomo lakini pia waendelee kutafuta fursa za
kuisaidia Tanzania ili nchi yao iweze kunufaika. Amewataka kila inapopatikana
fursa watoe taarifa nyumbani ili ziweze kufanyiwa kazi kwa haraka.
Naye, Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Cosato Chumi
aliwahakikishia viongozi hao wa diaspora kuwa Serikali imesikia ushauri na
maoni waliyoyatoa na itayafanyia kazi kwa haraka huku akimpongeza Mheshimiwa
Waziri Mkuu kwa namna ambavyo amekuwa akishughulikia hoja mbalimbali
zinazotolewa na wanadiaspora.
“Binafsi nimeambatana
na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika nchi nyingi na kote huko amekuwa akitatua
changamoto zinazojitokeza na kukwamua mambo yaliyokuwa yamekwama kwa muda mrefu
kama ilivyokuwa kwenye mikataba ya ushirikiano baina ya Tanzania na Belarus,
Nigeria na Ghana,” alisema.
Katika ziara hiyo ya
siku moja, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Cosato Chumi; Balozi wa Tanzania nchini
Kenya anayeiwakilisha Jamhuri ya Shelisheli, Dkt. Bernard Kibesse na maafisa
waandamizi wa Serikali.

0 Maoni