Katika juhudi za
kuboresha miundombinu na kuinua uchumi wa wakazi wa wilaya ya Mbinga, Meneja wa
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani humo, Mhandisi Oscar
Musa, amesema mradi wa Agri-Connect unaotekelezwa katika barabara ya
Utili–Mahande umefikia hatua muhimu ya ujenzi.
Mradi huo wenye urefu
wa kilomita 14.4 na thamani ya shilingi bilioni 16.5 ulianza kutekelezwa mwezi
Novemba 2024 na unatarajiwa kukamilika Mei 2026, ikiwa ni kipindi cha miezi 18.
Kwa sasa, kazi ya kuchonga na kufungua barabara yote imekamilika, huku ujenzi
wa madaraja saba ukiendelea sambamba na uwekaji wa tabaka la udongo ambapo
kilomita 8 tayari zimekamilika.
Mhandisi Musa amesema
kwamba mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi kutoka kampuni ya Ovans
Construction Ltd iliyoko Mbinga.
“Lengo kuu la mradi huu
ni kuwahudumia wananchi wa vijiji vya Utili, Mahande na Mbinga kwa ujumla.
Mradi huu unatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa pembejeo na mazao ya wakulima
hususan kahawa na mazao ya nafaka, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi
wa maeneo haya”.
Mhandisi Musa ameongeza
kuwa Wilaya ya Mbinga inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita
2,037, ambapo kilomita 45 ni za lami, kilomita 207 ni za changarawe na kilomita
1,780 ni za udongo. Kutokana na jiografia ya eneo hili kuna zaidi ya madaraja
300.
Awali, bajeti ya wilaya
kwa ajili ya barabara ilikuwa shilingi bilioni 1.7, lakini katika kipindi cha
Awamu ya Sita bajeti imeongezeka hadi kufikia bilioni 5.2,” ameongeza kusema.
Amesema kwamba ongezeko
hilo limewezesha ujenzi wa kilomita 8 za barabara ya lami, ufungaji wa taa mpya
53 na ufunguzi wa zaidi ya kilomita 300 katika halmashauri zote mbili za wilaya
hiyo.
Aidha, Mhandisi Musa
ameishukuru Serikali kwa ongezeko hilo la bajeti ambalo ni zaidi ya asilimia
200, akisema limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa mwaka wa fedha
2025/2026, TARURA Mbinga inatarajia kujenga madaraja ya mawe 12, kufanya
matengenezo ya barabara za kiwango cha lami kilomita 1.8, kufunga taa za
barabarani zipatazo 18 na kufungua barabara mpya kilomita 120 kwa kuweka
changarawe katika kilomita 36.
Katika kuhakikisha
ushirikishwaji wa wananchi, TARURA wilayani Mbinga imeendesha mafunzo kwa
vikundi kazi ambapo jumla ya washiriki 24 walihudhuria na vikundi vinne vimesajiliwa
rasmi. Vikundi hivyo tayari vimepata kazi katika awamu tofauti za miradi ya
barabara wilayani humo, hatua inayolenga kuongeza ajira na ushiriki wa jamii
katika maendeleo ya miundombinu.
Naye, Bw. Theofred
Komba, mkazi wa Utili amesema kwamba wanamshukuru Mhe. Rais kwa kuwajali
wananchi wake kwani ujenzi wa barabara hiyo utawasaidia kusafirisha mazao yao
pia kuwaondolea adha ya usafiri kwani awali walikuwa wakilipa shilingi 5000
lakini kwa sasa wanalipa 3000.
Bi. Leonia Komba mkazi
wa Utili amesema kukamilika kwa barabara hiyo itawasaidia wajawazito kufika kwa
wakati kwenye kituo cha afya tofauti na zamani ambapo ilikuwa ngumu kuwahi
huduma hususan kipindi cha mvua ilikuwa shida sana.




0 Maoni