Kura ndio
msingi wa maamuzi ya nchi, kura hutumika kuchagua chama kinachotoa ilani na
viongozi wanaowajibika kuitimiza. Kura yako haichagui tu Rais au Mbunge, bali
inakipa madaraka ya utekelezaji chama kinachoamini katika matumizi endelevu ya
rasilimali za maji, bahari, mito, maziwa, na mabwawa.
Umuhimu wa
Kura
Kwa kuwa kura
huwajibisha utekelezaji wa Ilani wananchi wanapaswa kufuatilia ilani hizo
kuzielewa na kutafakari Ilani za vyama mbalimbali kabla ya kuingia katika
sanduku la kura Oktoba 29.
Mathalani Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) 2025–2030
inaahidi mambo makubwa katika Uchumi wa Buluu, kama vile ujenzi wa Bandari ya
Uvuvi Bagamoyo na Kilwa, kuwezesha wavuvi kwa mikopo na vifaa vya kisasa, na
kuanzisha vituo vya ukuzaji viumbe maji.
Kwa hiyo
mwananchji kama ameridhika na maelezo haya maana yake kama anataka
kilichozungumzwa ataipatia Kura (idhini)
Chama Tawala kutumia rasilimali za Taifa kutekeleza ahadi hizi. Bila kura yako,
chama hicho hakiwi na nguvu za kisheria wala kisiasa kuendeleza meli za uvuvi
wa bahari kuu au kuimarisha masoko ya samaki na mialo. Kura ndiyo njia ya
kumfanya kiongozi ajisikie anafanya kazi kwa ajili ya wananchi na si kwa ajili
yake binafsi.
Hivyo kura
yako hutumika kutoa alama ya kupita au kufeli. Iwapo Serikali iliyopo
madarakani imetekeleza miradi mikubwa kama inavyoahidi, mfano, kutoa mikopo kwa
wakulima wa mwani na wavuvi au kujenga mabwawa, wananchi wanaweza kuendeleza
uwepo wake kwa kuipigia kura tena.
Ikiwa
utendaji hauridhishi, kura huipa nafasi chama kingine cha upinzani kuingia na
kujaribu kutekeleza ilani yao. Kwa hiyo, kura ndiyo mfumo wa usimamizi (check
and balance) unaodhibiti Chama Tawala; ndiyo inayoamua namna gani Chama Tawala
kitaendelea kuwepo—kwa kufanya vizuri au kuondolewa kwa kutofanya vizuri.
Uchumi wa
Buluu umeelezwa kama "zaidi ya mawimbi; ni dira ya uzalendo na
ubunifu." Miradi kama Bandari ya Bagamoyo inataka kufanya Taifa letu
kutumia rasilimali zake kwa hekima na maendeleo.
Kwa maneno
mengine vijana wanapopiga kura, wanathibitisha uzalendo wao kwa kuchagua
viongozi ambao wanaamini watalinda rasilimali za Taifa kwa ajili ya vizazi
vijavyo. Kura yako inalinda bahari, maziwa, na mito isitumiwe vibaya, na badala
yake iwe chanzo cha ajira, biashara, chakula na utajiri. Kura ndiyo inaweka
ulinzi wa kidemokrasia kuhakikisha ahadi za uwekezaji katika mabwawa na vizimba
vya samaki vinakuwa fursa za kibiashara na si maneno matupu.
Kwa kifupi,
kura yako haiamui tu mshindi wa uchaguzi; inatoa idhini ya kutekeleza maendeleo
ya Taifa na inakupa uwezo wa kuwawajibisha wale wote walioahidi kwamba Uchumi
wa Buluu ni dira ya mustakabali wa Tanzania.

0 Maoni