Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhe. Mbarak Alhaji Batenga,
ameweka wazi Mikakati Kabambe ya kuimarisha shughuli za uchimbaji madini
Wilayani humo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa
Kituo cha Umeme (Substation) chenye uwezo wa kuzalisha Megawati 90 hatua
inayolenga kupunguza changamoto za upatikanaji wa nishati hiyo kwenye shughuli
za madini na nyingine.
Katika mahojiano maalum na timu ya Madini Diary Oktoba 09
2025, Mhe. Batenga alisema kituo hicho kitajengwa katika eneo la Makongorosi – Chunya hivyo kitahudumia maeneo ya Chunya na Mkoa wa
Songwe, huku akitolea mfano wa Mgodi mpya wa Shanta- New Luika, Mtambo wa
uchenjuaji wa Anglo De Beers ambao upo mpakani mwa Chunya na Songwe na mgodi
mpya wa Porcupine North katika
eneo lililoongezwa baada ya upanuzi,
upo Chunya.
Alisema hivi sasa wilaya hiyo inatumia megawati 9 pekee huku
mahitaji halisi yakiwa si chini ya megawati 90, na kueleza, ‘’kupitia kituo
hiki, tutaanza kuzalisha megawati 45 – lengo ni kufanikisha uchimbaji wa kisasa
kwa gharama nafuu, na hivyo kuchochea uwekezaji zaidi. Wachimbaji wetu
wanahitaji sana umeme na hapa ninapokea maombi mengi sana ya kufikishiwa
nishati hiyo kwenye maeneo yao, na katika hili, nitalisimamia,” alisisitiza
Batenga.
Kutokana na mahitaji
hayo makubwa ya umeme hususan kwenye shughuli za uchimbaji, alitoa wito kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
kutoa kipaumbele cha kusambaza umeme kwenye maeneo yenye
shughuli za madini wakati wakipeleka maeneo
mengine kutokana na mahitaji makubwa jambo litakalosaidia kupunguza gharama za
uzalishaji na hivyo kuongeza uzalishaji na kueleza kwamba, upatikanaji wa nishati hiyo utasaidia kuvutia uwekezaji zaidi kutokana na wilaya hiyo
kubarikiwa utajiri wa rasilimali madini
na kugusia ujio wa kampuni ya uchimbaji
madini ya Anglo De Beers ambayo ina
baadhi ya leseni zake Chunya huku tayari ikiwa imeanza uchimbaji Songwe eneo la Mbangala.
Vilevile, alitoa shukrani kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kuweka
kuipa kipaumbele sekta ya madini na hususan wachimbaji wadogo,
na kueleza kwamba, zaidi ya leseni
1,500 zilitolewa kwa ajili ya wachimbaji
wadogo kwa wilaya hiyo na kutoa ombi la
kuendelea kutoa leseni zisizoendelezwa ili wale wenye nia ya kuziendeleza
wachimbe.
Katika hatua nyingine, aliiomba Wizara ya Madini kufanya
tafiti zaidi ili kugundua maeneo mapya yenye madini ili kuwawezesha wachimbaji
kuchimba pasipo kubahatisha na kupongeza kwa kutolewa mitambo ya uchorongaji
miamba. Kutokana na shughuli za uchorongaji kutokuwa nafuu, alishauri
kupatikana mitambo yenye gharama nafuu zaidi ili kuwezesha wachimbaji wadogo
kumudu gharama za utafiti, na kusema, ‘’ lakini sisi hatuchimbi tu dhahabu,
hivi sasa kuna kiwanda cha kuchenjua shaba hivyo
ninawaasa wachimbaji waanze kuangalia na madini hayo,’’ alisema.
Katika mazungumzo yake, akayataja maajabu
ya kipekee ya tarafa mbili
zinazounda wilaya hiyo za Kiwanja na Kipambawe, Batenga alisema, “kila
moja ni ya kipekee, tarafa ya Kiwanja ni
maalum kwa shughuli za madini na
Kipambawe mahususi kwa kilimo cha tumbaku. Madini hayapo kabisa
Kipambawe na hakuna uchimbaji huko na tumbaku haistawi kabisa eneo la Kiwanja huko kuna kilimo kwa kiasi kidogo tu
kwa mazao ya chakula,’’ alieleza.
Akizungumzia mchango wa sekta hizo wilayani humo, alisema
hivi sasa Wilaya ya Chunya inachangia asilimia 60 ya fedha za maendeleo kwenye
mfuko Mkuu wa Serikali, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka asilimia 40 kwa miaka ya
nyuma. “Tunatarajia kuwa ndani ya miaka mitano ijayo, Chunya itachangia hadi
asilimia 80, kutokana na mapato ya madini na tumbaku, na kuongeza kuwa hivi
sasa Halmashauri, inanufaika kwa kupata kiasi cha shilingi bilioni 5, kutokana
na mapato ya sekta hizo mbili kuu, madini na tumbaku.
#Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri


0 Maoni