Majimbo matatu ya India yamepiga marufuku matumizi
ya dawa ya kikohozi baada ya watoto wasiopungua tisa kufariki dunia, wakidaiwa
kufa kutokana na kutumia dawa hiyo, mamlaka zimesema.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya ya India,
sampuli za dawa ya kikohozi aina ya Coldrif, inayotengenezwa na kampuni ya
Sresan Pharma iliyoko Tamil Nadu, kusini mwa India, zilionyesha kuwa na
kemikali aina ya diethylene glycol (DEG).
DEG ni kemikali hatari inayotumika viwandani, ambayo
ni sumu kali na inaweza kusababisha madhara makubwa kiafya hata kwa kiasi
kidogo inapotumiwa na binadamu.
“Tumeona kuwa sampuli hizo zina kiwango cha DEG
kilichozidi kikomo kinachokubalika,” ilisema taarifa ya wizara hiyo.
Waziri Mkuu wa jimbo la Madhya Pradesh, Mohan Yadav,
ambako ndiko vifo vingi vimeripotiwa, alisema: “Uuzaji wa dawa hii umepigwa
marufuku kote katika jimbo la Madhya Pradesh.”
Marufuku hiyo imeungwa mkono pia na majimbo mengine
mawili kufuatia tahadhari hiyo ya kiafya.
Dawa za kikohozi zinazozalishwa India zimekuwa
zikitiliwa shaka katika miaka ya hivi karibuni, zikihusishwa na vifo duniani,
vikiwemo vifo vya watoto 70 Gambia mwaka 2022.
0 Maoni