Wananchi wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara wameipongeza
na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa kwa kuwajengea vizimba vya kuzuia mamba kuwadhuru wakati wa
kuchota maji ziwani na kufanya shughuli zingine pembezoni mwa Ziwa Victoria
ikiwemo kufua na kuoga.
Wamesema hayo jana Oktoba 5, 2025 kwa nyakati
tofauti wakati timu ya wataalam kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka
ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ilipotembelea maeneo ya vizimba
hivyo.
Akizungumza katika ziara hiyo,Mkazi wa Mwiseni,kata
ya Butimba, Bi. Gabaseki Gervaz amesema
wamefurahi sana kupata kizimba kutokana na changamoto walizokuwa wanakutana
nazo mwanzoni za kukamatwa na mamba wanapofanya shughuli zao pembezoni mwa
ziwa.
"Serikali baada ya kuona tunateseka kutokana na
vifo kila mwaka kwa kuuliwa na mamba ikajenga kizimba hiki" amesema Bi.
Gervas na kuiomba Serikali kuongeza vizimba vya ziada kwa ajili ya jinsia ya
kiume na mifugo.
Naye, Bw. Tabingwa Charles Kasao naye mkazi
kitongoji cha Nampangala kata ya Kisorya ,Bunda mkoani mara ameishukuru
Serikali kwa kujali wananchi na kujenga kizimba katika eneo hilo na kuepusha
vifo vya wananchi wakiwemo wanafunzi wanaotumia ziwa hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwiseni,
Bw. Msiba Chiharata amesema kutokana na faida za vizimba katika kuzuia mamba
wameweka adhabu kwa wananchi wanaojaribu kuharibu eneo la Kizimba.
"Tumeweka adhabu kwa mtu yeyote atakayefanya
uharibifu wa aina yeyote ile iwe ni kuanika nguo au kuingiza mifugo eneo la
vizimba faini ni shilingi laki moja" amesema Bw.Msiba.



0 Maoni