Tukiwa
tunakaribia Uchaguzi Mkuu, wito mkubwa unatolewa kwa Watanzania wote kulinda
hazina yetu ya Amani na Utulivu.
Demokrasia
haina maana bila amani. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuhakikisha kuwa, licha
ya tofauti zetu za kisiasa, tunadumisha heshima, tunafanya siasa safi, na
tunakubali matokeo yanayotokana na sanduku la kura.
Tukumbuke
kwamba nchi yetu ni moja, na upigaji kura ni zoezi la muda mfupi, lakini amani
ni urithi wa kudumu kwa vizazi vijavyo.
Mmoja wa
waimbaji wa Injili Christina Shusho ambaye alishawahi kuwa katika kamati ya
Amani nchini Tanzania wakati wa Utawala wa awamu ya nne anasema kwamba kila
siku ni lazima wananchi lazima watambue umuhimu wa uhai na kuenzi Amani.
Anasema
ni kazi kubwa kuenzi Amani lakini ni rahisi kubomoa kama watu hawatakuwa
waangalifu katika kauli na matendo yao na kwamba bila Amani hakuna shughuli
nyoiyote itakayostawi.
Uchaguzi Sio Vita, Ni Maamuzi
Ni muhimu
kwa Vyama vya Siasa na Wafuasi wao kuweka mbele maslahi ya Taifa. Uchaguzi si
vita, bali ni mchakato wa kidemokrasia wa kuchagua viongozi tunaowaamini.
Badala ya kuruhusu jazba na chuki, tunapaswa kujikita katika hoja, mijadala
yenye tija, na kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
Jeshi la
Polisi na vyombo vingine vya ulinzi vimeapa kulinda raia na mali zao, na
vinahitaji ushirikiano wetu ili kudumisha utulivu katika kipindi chote cha
kampeni, upigaji kura na baada ya matokeo. Tutumie fursa hii ya kidemokrasia
kwa ustaarabu na utulivu.
Jukumu la Kiongozi na Mwananchi
Viongozi
wa kisiasa wanalo jukumu la kutoa hotuba zenye kuhamasisha umoja na kuacha
kauli zinazochochea mgawanyiko au vurugu. Kadhalika, kila mwananchi anawajibika
kuepuka kueneza taarifa za upotoshaji (fake news) au uchochezi kupitia mitandao
ya kijamii. Amani huanzia kwetu.
Kanisa
Katoliki kupitia viongozi wake wakuu akiwemo Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Dar es
Salaam Thadeus Ruwaich amesisitiza wananchi kutoyumbishwa na taarifa zisizo
sahihi na kwamba kanisa halina ugomvi na serikali na ni vyema wananchi
wakatimiza sharia zilizopo.
Kwa
kuhakikisha kila hatua ya uchaguzi inakwenda kwa utulivu, Watanzania wanapaswa
kutoaa heshima kwa katiba ambayo ndiyo
inaweka msingi thabiti wa maendeleo endelevu. Tanzania itabaki salama na imara
ikiwa wananchi wataweka kura zao kama haki yao, na amani kama wajibu wao.

0 Maoni