Mkuu wa
Wilaya ya Rufiji, Luteni Kanali Fredrick Komba ameipongeza Wakala ya Barabara
za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kurejesha mawasiliano ya miundombinu ya
barabara katika wilaya yake.
Amesema
wilaya ya Rufiji kwa mwaka 2023/2024 ilipata mafuriko ambayo yaliathiri ÅŸana
miundombinu ya barabara katika tarafa ya Mohoro, Ikwiriri pamoja na Mkongo.
“TARURA
imeweza kufanya kazi nzuri kwa nafasi yake kwani kwa muda mfupi imeweza
Kurekebisha hitilafu zilizotokana na mafuriko.”
Akitolea
mfano Luteni Kanali Komba amesema TARURA imejenga barabara mpya za lami, ujenzi
wa daraja la Mohoro lenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni 17 ambalo
linaunganisha vijiji viwili vya Ndundutawa na King’ongo zinazounganisha Makao
Makuu ya Tarafa ya Mohoro na kijiji cha Kipoka katika Kata ya Chumbi.
“Naipongeza
Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutekeleza miradi mingi ya TARURA kwenye wilaya
ya Rufiji.”
“Mimi na
wananchi tunaweza kusafiri mahali popote kwenye wilaya hii, ujenzi wa
miundombinu umeleta matumaini makubwa
kwa wananchi wa Rufiji,” ameongeza.
Amesema
Serikali imeonesha dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha
miundombinu ya barabara inakua thabiti na wananchi kuweza kusafirisha mazao
yao.
Kwa
upande wake, Meneja wa TARURA wilaya ya Rufiji, Mhandisi Nicolaus Ludigery
amesema kwamba miradi yote inayotekelezwa katika wilaya ya Rufiji inaenda
kuwarahisishia wananchi shughuli za kijamii na kiuchumi.
Amesema
barabara nyingi zilipata athari kubwa kutokana na mafuriko na kimbunga Hidaya,
hivyo wamejipanga kuhakikisha miradi yote inakamilika kama ilivyokusudiwa.
Naye, Bi.
Saida Mwilu mkazi wa Ikwiriri amesema ujenzi wa barabara za lami kwenye mji wa
Ikwiriri zimewaletea manufaa makubwa hususan kwa wajasiriamali ambao hutembeza
bidhaa zao mitaani kwani awali kipindi cha mvua kulikuwa na madimbwi ya maji na
kuongeza kwamba taa za barabarani zitakapowekwa itawasaidia kufanya biashara
hadi usiku na kwa usalama.
Pia, Bw.
Malik Kitala mwendesha bodaboda ameishukuru Serikali kwa kuwatengenezea
barabara kwani awali kutokana na ubovu wa barabara hasa kipindi cha mvua nauli
zilikuwa juu.



0 Maoni