Idara ya
Uhamiaji nchini imetoa taarifa ikieleza kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Wegesa Heche, ameondoka nchini kupitia
mpaka wa Sirari, wilayani Tarime, bila kufuata taratibu na kanuni za uhamiaji.
Kupitia
taarifa rasmi iliyotolewa, Oktoba 18, 2025, na kusainiwa na Paul Mselle,
msemaji wa Idara hiyo, tukio hilo lilitokea katika Kituo cha Uhamiaji cha
Sirari, mkoani Mara, ambapo Heche alivuka mpaka na kuingia nchini Kenya kinyume
na masharti ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54.
“Idara ya
Uhamiaji inapenda kuujulisha umma kuwa leo tarehe 18 Oktoba, 2025, katika Kituo
cha Uhamiaji cha Mpaka wa Sirari mkoani Mara, Mheshimiwa John Wegesa Heche
ameondoka nchini kwa kuvuka mpaka na kuingia nchi jirani bila kufuata taratibu
na kanuni za uhamiaji zilizoundwa chini ya Sheria ya Uhamiaji Sura ya 54,”
imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha,
Idara hiyo imetoa wito kwa Watanzania na wageni wanaotoka au kuingia nchini
kuhakikisha wanafuata taratibu zote za kisheria zinazohusu uingiaji, ukaaji na
utokaji wa watu nchini, ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.
Taarifa
hii imekuja saa chache baada ya Chama cha Chadema kudai kuwa Heche amezuiwa
kusafiri kwenda nchini Kenya kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa
Kenya, Raila Odinga, yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 19,
2025, kijijini Bondo.


0 Maoni