Wakati
mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa 2025 ukiendelea, Mmoja wa viongozi wa kimila
nchini, Chifu Mussa Bwakila Lukwele IV, ametoa wito mzito kwa Watanzania, hasa
kizazi kipya, kulinda na kuienzi amani iliyoisukuma Tanzania kuwa 'Kisiwa cha
Amani' barani Afrika.
Chifu
Lukwele, ambaye ni Chifu Mkuu (Paramount Chief) wa Waluguru wa Himaya ya Jadi
ya Choma, amempongeza kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia
misingi imara ya upendo, umoja, utulivu, na mshikamano iliyoachwa na
watangulizi wake.
Akirejelea
tafiti za hivi karibuni za taasisi za kimataifa, ikiwemo Shirika la Utangazaji
la Uingereza (BBC), Chifu Lukwele alibainisha kuwa Tanzania imeng'ara kwa kuwa
nchi salama zaidi Afrika Mashariki.
"Bila
hiyana hatuna budi kumpongeza Mkuu wa nchi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,
kwa kusimamia misingi iliyopo awamu zote," alisema Lukwele.
Ripoti
hizo zimeiweka Tanzania katika nafasi nzuri, huku ikielezwa kuwa ina viwango
vichache vya uhalifu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, hali inayotufanya kuwa
'Barua Inayosomeka' kwa mataifa mengine. Utafiti wa Global Peace Index (GPI) wa
2025 pia unaiorodhesha Tanzania katika nafasi ya 73 kwa kuwa nchi salama zaidi
duniani.
Onyo kwa
‘Kizazi Z’ Dhidi ya Siasa za Uhasama
Akihofia
hali ya sasa ya kisiasa, Chifu Lukwele alielekeza wito maalum kwa vijana wa
kizazi kipya (‘Generation Z’), ambao hawajawahi kushuhudia vita, akiwasihi
'wasichukulie poa' neno vita.
"Vijana
wachache kizazi hiki hawajui nini maana ya machafuko, tunawasihi wasikubali
kushawishiwa na wanasiasa wasiolitakia mema Taifa hili," alisema, na
kuwasihi vijana watazame hali ilivyo kwa majirani zetu, ambapo Tanzania imebaki
kuwa 'kimbilio la walioharibikiwa'.
Alisisitiza
kuwa kizazi kichanga kipo hatarini kuburuzwa kwenye giza kutokana na uzoefu mdogo
wa maisha na upeo finyu wa kuchanganua mambo.
Maisha
Baada ya Uchaguzi na Siasa za Hoja
Chifu
Lukwele alikemea wanasiasa wanaotumia matatizo ya vijana, ikiwemo ukosefu wa
ajira au mitaji, kuwachochea wavuruge amani kwa maslahi yao binafsi ya kisiasa.
Aliwataka
wanasiasa kutumia kipindi hiki cha kampeni kunadi sera na kujenga hoja zenye
kuingia akilini mwa wapiga kura, badala ya kupanda mbegu za chuki, uhasama,
mifarakano, na kushambuliana binafsi.
"Ikumbukwe
kuwa, KUNA MAISHA BAADAA YA UCHAGUZI ambayo ni marefu zaidi kuliko miezi miwili
ya kampeni na siku yenyewe ya kupiga kura," alisisitiza Chifu Lukwele.
Majirani
Watikisika: Kenya na Uganda Zatajwa Kushuka
Kinyume
na hali ya Tanzania, ripoti za kimataifa zinaonesha majirani wamekuwa na hali
mbaya ya usalama:
Kenya:
Inaongoza kwa kutokuwa salama Afrika Mashariki, ikiorodheshwa nafasi ya 14
barani Afrika.
Uganda:
Imetajwa nafasi ya 23 kwa nchi isiyo salama, na kuifanya ya pili katika Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Aidha,
ripoti ya GPI inaeleza kuwa kiwango cha amani Kusini mwa Jangwa la Sahara
kimepungua kwa wastani, huku nchi tatu kati ya kumi zenye migogoro mikubwa
zaidi duniani zikipatikana kwenye eneo hili. DRC, Sudan Kusini, Mali, Burkina
Faso, Somalia, CAR, na Nigeria zimetajwa kuwa miongoni mwa mataifa saba (7)
yenye hali mbaya zaidi ya usalama barani Afrika.
Wito wa
Kuelimisha Kuanzia Familia
Ili
kudumisha hali hii ya kipekee ya amani, Chifu Lukwele alihitimisha kwa kutoa
wito kwa kila Mzazi na Mlezi: "Sema na Mwanao."
Alisisitiza
kuwa jitihada za Rais Samia za kulinda amani hazina budi kuungwa mkono kwa
kutoa elimu kubwa zaidi kwa kundi la vijana, kuanzia ngazi ya familia, ili
kuwawezesha kutambua matokeo mabaya ya vurugu na kukataa kuburuzwa na siasa za
uchochezi.

0 Maoni