Zaidi ya
watalii 500 walifurika jana Oktoba 18, 2025, katika Bustani ya Wanyamapori
Tabora (Tabora Zoo) kushiriki katika Tamasha la Nyamapori Choma lililoandaliwa
na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Magharibi.
Tamasha
hilo lililolenga kuhamasisha utalii wa ndani pamoja na matumizi endelevu na
halali ya rasilimali za wanyamapori, limevutia watalii kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya
nchi, likihudhuriwa na viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Wilaya za Tabora
na Uyui, wananchi wa Mkoa wa Tabora na mikoa jirani, pamoja na wageni kutoka
mataifa mbalimbali duniani.
Wananchi
waliohudhuria tamasha hilo wameipongeza TAWA kwa ubunifu wa kuandaa tukio hilo,
wakieleza kuwa limewapa fursa ya “kuonja ladha ya matunda ya uhifadhi” unaotekelezwa
na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii Kwa kuhakikisha wananchi
wananufaika na rasilimali hizo Kwa njia halali bila kuathiri uhifadhi endelevu.
Kwa siku
nzima ya leo, anga la Tabora Zoo lilitawaliwa na nderemo, shamrashamra za
muziki wa asili, na harufu murua ya nyama pori choma zilizokuwa zikigeuzwa kwa
ustadi na wapishi mahiri. Wageni wakipata fursa ya kuonja ladha ya nyama pori
huku wakijifunza kuhusu umuhimu wa uhifadhi endelevu wa wanyamapori kama sehemu
ya utalii wa ndani na urithi wa rasilimali za taifa.
Tamasha
hilo limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuelimisha, kuburudisha, na kuhamasisha
jamii kuenzi thamani ya rasilimali wanyamapori kupitia utalii
utalii wa ndani.



0 Maoni