Dkt. Mwinyi aahidi kuendelea kuwawezesha wajasiriamali na kuimarisha miundombinu ya masoko

 

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kujenga masoko katika kila wilaya na mkoa ili kuandaa mazingira bora zaidi kwa wajasiriamali nchini.

Akizungumza  na makundi mbalimbali ya Wajasiriamali, waendesha bodaboda na bajaji, Wajane, Wavuvi na Wakulima katika mkutano wa hadhara wa  kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Kihinani, Mkoa wa Mjini Magharibi leo tarehe 18 Oktoba 2025, Dkt. Mwinyi amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kufanya biashara katika mazingira salama, ya kisasa, na yenye tija.

Halikadhalika, Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwapatia wajasiriamali mafunzo ya biashara na alama za ubora ili bidhaa zao ziweze kufikia viwango vya kimataifa na kuhimili ushindani wa soko la kikanda na kimataifa.

Kuhusu tozo za masoko, Dkt. Mwinyi amesema Serikali italifanyia kazi suala hilo kwa lengo la kuhakikisha wajasiriamali wanatozwa viwango rafiki vinavyorahisisha shughuli zao za kila siku. Aidha, aliahidi kujenga vituo vya mabasi vyenye maeneo maalum kwa bodaboda, na kutoa mikopo nafuu kwa wajasiriamali baada ya kurasimisha biashara zao.

Katika sekta ya kilimo, Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuimarisha skimu za umwagiliaji, kuwapatia wakulima pembejeo, mbolea za bei nafuu, na mafunzo kupitia mabwana shamba ili kuongeza uzalishaji na kujitosheleza kwa chakula.

Kwa upande wa uvuvi, amesema Serikali itaendeleza ujenzi wa masoko ya kisasa na madiko, pamoja na viwanda vya kusarifu samaki katika eneo la Fungu Refu kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya baharini, sambamba na ujenzi wa gati jipya katika eneo la Kihinani.

Akizungumzia masuala ya kijamii, Dkt. Mwinyi amesema Serikali itaweka adhabu kali kwa wazazi wanaotelekeza watoto wao ili kukomesha tabia hiyo, na ameahidi kuwawezesha wajane kupitia mikopo isiyo na riba na mafunzo ya kujikwamua kiuchumi.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka utaratibu mzuri wa uendeshaji wa masoko ili yawe safi, rafiki kwa wajasiriamali, na kulinda haiba ya miji ya Zanzibar.

Vilevile, Dkt. Mwinyi ametangaza kuwa tarehe 29 Oktoba 2025, siku ya kupiga kura, itakuwa siku ya mapumziko, na amewataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu huo.

Kabla ya kuanza kuhutubia wananchi, Dkt. Mwinyi alipiga simu kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Bi. Fatma Hamad Rajab, aliyekuwa katika Uwanja wa New Amaan Complex ambako timu za KMKM na Azam FC zilikuwa zikicheza mechi ya raundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika. Kupitia salamu hizo, aliwatakia mchezo mwema na kuwakumbusha wanamichezo pamoja na wananchi wote umuhimu wa kujitokeza kupiga kura.

Akiwahitimishia wananchi wa Kihinani, Dkt. Mwinyi ameomba kupewa tena ridhaa ya kuiongoza Zanzibar kwa awamu nyengine, akiahidi kuendeleza juhudi za kuleta maendeleo makubwa zaidi kwa wananchi wote wa Zanzibar.



Chapisha Maoni

0 Maoni