Watalii wa ndani 800 kutoka Chama
cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) wametembelea Hifadhi ya
Taifa Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za
kukuza Utalii wa Ndani na kutambua fursa za uwekezaji zinazopatikana katika
sekta ya utalii.
Katika ziara hiyo iliyofanyika
jana, wageni hao walipata fursa ya kushuhudia vivutio mbalimbali vilivyomo
ndani ya hifadhi, ikiwemo maporomoko ya maji, hali ya hewa ya kipekee pamoja na
mimea ya aina mbalimbali inayopamba mandhari ya Mlima Kilimanjaro, maarufu
duniani kama “paa la Afrika”.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo,
Katibu wa TUGHE Henry Mkunda alisema, “Watalii wetu wamefurahishwa na mandhari
ya kipekee ya Mlima Kilimanjaro na vivutio vilivyomo ndani yake. Ziara hii
imetupa uelewa mkubwa zaidi wa thamani na uzuri wa urithi huu wa dunia.”
Kwa upande wake, Naibu Kamishna
wa Uhifadhi TANAPA, Steria Ndaga, kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi TANAPA,
alisema, “Tunawapongeza viongozi na wanachama wa TUGHE kwa kuunga mkono
jitihada za kutangaza utalii wa ndani. Ni wajibu wetu sote kuhakikisha
tunalinda na kutangaza vivutio hivi vya pekee. Napenda kuwasisitiza Watanzania
wote kutembelea hifadhi zetu, kwani kufanya hivyo ni kuongeza pato la taifa na
kuchangia ajira kwa vijana.”
Aidha, aliwahamasisha wananchi
kuwekeza katika sekta ya uhifadhi kwa kusema: “Fursa za uwekezaji zipo nyingi
ndani ya Hifadhi za Taifa. Tukishirikiana kwa pamoja, watanzania wanaweza
kunufaika kiuchumi huku taifa likipata mapato endelevu na kuimarisha maendeleo
ya kijamii.”
Naye Kamishna Msaidizi wa
Uhifadhi anayesimamia Kitengo cha
Maendeleo ya Biashara TANAPA, Jully Bede Lyimo, aliwataka wageni hao
kuendeleza utalii rafiki wa mazingira akisisitiza kuwa shughuli za utalii ni
lazima tuzingatie uendelevu, faida za utalii wa ndani ni nyingi; unaongeza
mapato ya serikali, unachochea ajira hasa kwa vijana, unakuza biashara ndogo
ndogo, unajenga uzalendo na uelewa wa wananchi kuhusu thamani ya urithi wetu wa
asili na vilevile unapunguza utegemezi wa watalii wa kigeni pekee. Hivyo, kila
mmoja wetu anaposhiriki katika utalii wa ndani anachangia moja kwa moja katika
maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii.
Nae kaimu Mkuu wa Hifadhi ya
Taifa kilimanjaro afisa uhifadhi mkuu Amri Mtekanga kwa niaba ya Mkuu wa
Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro aliwakaribisha watalii hao na kuwaelezea vivutio
vilivyopo ndani ya Hifadhi hiyo
iliyobeba hivi Karibuni tuzo ya utalii duniani kama Hifadhi bora zaidi barani
Afrika yenye milima na kutoa taratibu za upandaji wa Mlima Kilimanjaro.
Ziara ya TUGHE katika Hifadhi ya
Taifa Kilimanjaro ni mfano halisi wa mshikamano wa watanzania katika kuunga
mkono sekta ya utalii. Huku dunia ikiendelea kuhesabu siku kuelekea maadhimisho
ya Siku ya Utalii Duniani, TANAPA inawakaribisha Watanzania wote kutembelea
hifadhi za taifa ili kujivunia urithi wa asili, kuhamasika kuwekeza, na
kushiriki katika kujenga mustakabali endelevu wa
utalii wa nchi yetu.
0 Maoni