Mgombea urais kwa tiketi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema chama hicho hakina
mashaka katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu kwa sababu mambo
mengi makubwa yamefanyika.
Ametoa kauli hiyo Septemba 18,
2025 akihutubia maelfu ya wananchi katika Viwanja vya Hamburu, Nungwi Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
"CCM tuna ujasiri,kuja kwenu
kuomba kura na ujasiri huu unatokana na kwamba tumefanya mambo makubwa,"
Dkt. Samia aliwaambia maelfu ya watu aliohudhuria mkutano huo.
Ameongeza: "Ndiyo maana
tunakuja kwenu kwa kujiamini kuomba kura, mtuchague tena ili twende tufanye
mambo makubwa zaidi kama alivyosema Dkt. Mwinyi."
Awali, mgombea urais wa Zanzibar
na Rais wa visiwa hivyo, Dkt. Hussein Mwinyi alieleza mambo mengi makubwa
yaliyofanywa na serikali yake pamoja na ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Aidha, Dkt. Samia amesema
wakipewa ridhaa, Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya
Mapinduzi ya Zanzibar zitaweka mazingira yatakayokuza kipato cha mwananchi
mmoja mmoja.
Amesema moja ya ahadi ya CCM ni
kuendelea kukuza uchumi na kipato cha mwananchi mmoja mmoja hatua ambayo
itawezesha nchi kujitegemea.
"Katika kujenga taifa linalo
jitegemea, hatutafika huko mpaka kila mtu ndani ya Tanzania yetu, kila kijana
awe na shughuli inayompa kipato yeye mwenyewe asimame kama mtu mmoja,
ajitegemee halafu kwa ujumla wetu tunaweza kujitegemea," alifafanua Dkt.
Samia.
"Na hii ndio kazi
tunayoiendea, tutakachokifanya ni kuandaa mazingira kwa vijana wetu kwa
Watanzania kuweza kuwa na shughuli za kufanya, kuingiza kipato ili kila mmoja
ainue ustawi wa maisha yake," alibainisha.
Ameongeza kuwa matokeo ya ukuaji
uchumi na utekelezaji ahadi za CCM kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita,
umeonekana dhahiri uwezo wa Dkt. Mwinyi katika kuwaongoza Wazanzibari.
Ameeleza kuwa ukuaji uchumi kwa
Tanzania Bara umeongezeka kwa asilimia sita huku Zanzibar ukiwa juu zaidi kwa
asilimia 7.1 kwa mwaka.
"Zaidi uchumi umekuwa hata
mifukoni kwa kila mwananchi. Wakati nilipokuwa nikiwasili Nungwi nilikuwa
nikitazama kila pande na kujionea namna ambavyo kumejengeka nyumba nzuri za
makazi, biashara zinafanyika na mambo yanaenda vyema kwa amani na
utulivu," lisema Dkt. Samia.
Akizungumzia pia ukuaji wa sekta
ya utalii Bara na Zanzibar, na kuwainua wananchi wa hali ya chini kupitia Mfuko
wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Ameahidi kuendelea na utekelezaji
wa miradi kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na kuimarisha uchumi wa buluu
hususani uvuvi katika bahari kuu na suala la mafuta na gesi.
Alisema pande mbili za Muungano
zimeshirikiana kukuza uhusiano wa kidiplomasia na kukuza jina la Tanzania.
Na. Aboubakary Liongo- Mkuu wa
Kitengo cha Habari na Mawasiliano Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM
0 Maoni