Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, amewataka Mawakili wa Serikali kuyatumia maarifa wanayoyapata kupitia mafunzo ya Hifadhi ya Jamii ili kuhakikisha kuwa sheria na kanuni za hifadhi ya jamii zinatekelezwa kwa ufanisi na kulinda haki na maslahi ya wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii nchini.
Mhe. Johari ametoa wito huo
Septemba 18, 2025, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu Hifadhi ya
Jamii kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa
Watumishi wa Umma (PSSSF) yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu
Nyerere, Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
huo, Mwanasheria Mkuu amesema kuwa mafunzo hayo yatakuwa chachu ya kuongeza
ujuzi kwa Mawakili wa Serikali katika maeneo mbalimbali ya kisheria, hususan
yanayohusiana na Hifadhi ya Jamii. Alizitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni
pamoja na Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma [Sura ya 371],
Sheria ya Mikataba [Sura ya 345], Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini [Sura ya
366], pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Fedha na Uwekezaji.
“Ni matarajio yangu kuwa mafunzo
haya yatajikita katika maeneo muhimu ya kisheria na kiutawala, ikiwemo muundo
wa kisheria wa PSSSF, majukumu yake ya msingi, pamoja na haki na wajibu wa
wanachama, wastaafu na wategemezi wao,” amesema Mhe. Johari.
Aidha, Mwanasheria Mkuu
amebainisha kuwa mafunzo hayo yatawasaidia Mawakili wa Serikali kuwa na uelewa
mpana wa namna ya kushughulikia masuala ya kisheria yanayohusu Mfuko wa PSSSF
kwa kutumia mbinu za usuluhishi na majadiliano, badala ya kusubiri migogoro
ifikishwe mahakamani.
“Mbali na kupunguza mashauri
yasiyo ya lazima, mafunzo haya pia yatawezesha kuwekwa kwa misingi imara ya
kisheria katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za Mfuko, pamoja na
kuimarisha uhusiano kati ya PSSSF na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa
manufaa ya Taifa,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, Mhe.
Johari amewataka Mawakili wa Serikali wanaoshiriki mafunzo hayo kuwa na ari ya
kujifunza na kuhakikisha kuwa maarifa wanayoyapata yanatumika kikamilifu katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Tunapozungumzia hifadhi ya
jamii, tunazungumzia maisha ya watumishi kabla na baada ya kustaafu. Ni wajibu
wetu kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inalindwa kwa mujibu wa sheria,” amesisitiza.
Mafunzo hayo yanaendelea kwa siku mbili na yanatarajiwa kuongeza tija katika usimamizi wa masuala ya hifadhi ya jamii nchini.
0 Maoni